Farid: Ilikuwa lazima tushinde

WINGA wa Yanga asiyetajwa sana na mashabiki wa timu hiyo, Farid Mussa amesema kujiamini na ubora wa kikosi chao msimu huu ndio siri ya bao la ushindi walilolipata.

Farid ndiye aliyetoa pasi ya bao lililofungwa na Fiston Mayele ameliambia Mwanaspoti, haikuwa rahisi kwake kufanya vilekutokana na presha ya mashabiki.

“Nimejisikia furaha kupata nafasi ya kucheza kwenye mchezo mkubwa wenye presha kilichonibeba ni kujiamini na kufuata nilichoelekezwa na mwalimu,” alisema Farid na kuongeza;

“Ubora wa kila mmoja na timu kucheza kwa ushirikiano ndio siri ya kupata matokeo tumeingia uwanjani kwa kuamini tunaweza tukifanya kwa ushirikiano na ndio kilichotokea.”

Farid alisema kupoteza michezo yao mitatu mfululizo kuanzia mechi dhidi ya Zanaco mchezo maalum kwa kutambulisha kikosi chao cha katika ‘Wiki ya Mwananchi’ na michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United kumewapa chachu ya kuingia wakiwa na uchu wa kusaka matokeo.

“Tumejeruhiwa mara tatu hatukutaka kukubali kuwa timu ya kupoteza michezo mfululizo na huu ni muhimu kwetu kwani tumekutana na mtani na ulikuwa ni mchezo wa heshima na ngao tuliohitaji ndio maana tumepambana dakika zote na Mungu alikuwa upande wetu.” alisema.

“Tumekuwa na mwanzo mzuri hatujaridhika na Ngao, tunaendelea na mapambano, kwani tunahitaji mataji zaidi na kutafuta nafasi kimataifa tuliyoipoteza tukiwa na kiu,” aliongeza.