EXCLUSIVE: MOLOKO ATANGAZA VITA

Muktasari:

WAKATI Yanga ikimuuza winga wao mwenye kasi, Tuisila Kisinda kwa klabu ya RS Berkane ya Morocco, mashabiki wa timu hiyo walichanganywa na uamuzi huo wa uongozi wakijiuliza wanauzaje silaha kama hiyo wakati wakiwa vitani? Hii ni kwa vile walivutiwa na soka lake la kasi lililozitesa timu pinzani.

WAKATI Yanga ikimuuza winga wao mwenye kasi, Tuisila Kisinda kwa klabu ya RS Berkane ya Morocco, mashabiki wa timu hiyo walichanganywa na uamuzi huo wa uongozi wakijiuliza wanauzaje silaha kama hiyo wakati wakiwa vitani? Hii ni kwa vile walivutiwa na soka lake la kasi lililozitesa timu pinzani.

Lakini baada ya siku chache akatua mbadala wake, kisha wakamuangalia wakaanza kupata wasiwasi kwa kumchukulia poa. Hata hivyo kumbe jamaa alikuwa hajawasha gari lake na sasa wameanza kuona moto na kuukubali mziki wake. Hapa tunamzungumzia Jesus Moloko.

Moloko amecheza mechi zote za Yanga msimu huu, lakini hizi tatu za hapa nyumbani za Ligi Kuu ameonyesha uwezo mkubwa akifanikiwa pia kutupia nyavuni bao moja.

Mwanaspoti limefanya naye mahojiano maalumu na kuweka wazi baadhi ya mambo yanayohusu maisha yake na ishu za soka, lakini akifichua kuwa kwa mziki uliopo Jangwani haoni kwa nini wasibebe makombe baada ya kuanza na Ngao ya Jamii wakiifumua Simba bao 1-0.

Pia amekichambua kikosi cha Simba akikilinganisha na alivyovaana nao misimu miwili iliyopita enzi hizo akiwa AS Vita ya DR Congo na kilivyo sasa, huku akieleza jinsi lugha inavyomsumbua, ingawa anakiri anainjoi maisha kwa namna mashabiki wa Yanga walivyompokea na kumpa heshima. Endelea...!

MAISHA YA BONGO

Moloko anaelezea kuwa Tanzania anasema ni nchi nzuri. Anafurahia namna mashabiki wanavyomuunga mkono na ukarimu waliomuonyesha unaompa nguvu ya kuipambania Yanga kutwaa mataji msimu huu.

“Walianza kunionyesha ushirikiano kabla sijaanza kucheza, jambo linalonipa moyo wa kupigania furaha yao kuwa endelevu kwa kufanya kazi wanayoitarajia kutoka kwangu,” anasema mchezaji huyo akielezea namna alivyofika na kukomaa na msosi wa chipsi pekee.

Anasema wakati anafika alikutana na changamoto ya chakula kilichompa shida kukizoea hasa wiki za mwanzo, lakini kwa sasa hakuna kinachomsumbua na anataja chipsi kuku kuwa kipenda roho chake.

“Sina maana kwamba hizo chipsi kuku nakula mara kwa mara, ila ni kwa hamu, kwani ni chakula kinachopikwa vizuri sana na kitamu, ila mwanzoni ndio kilikuwa chakula changu vingine vilikuwa vinanishinda.”

MKWANJA WAMVUTA

Moloko anasema hakuwahi kuwa na wazo wala kufikiria kama kuna siku angekuja kucheza soka nchini Tanzania, lakini alilazimika kuja baada ya kupata ushawishi wa mkwanja kutoka kwa mabosi wa Yanga.

Anasema ushawishi huo ulimfanya afanye uamuzi wa haraka kuja nchini na hajutii.

“Sikujua kama kuna siku ningekuja Tanzania kucheza hapa, lakini ghafla niliambiwa na meneja wangu kwamba Yanga wananihitaji na waliniwekea fedha nyingi. Wakati huo nilishaambiwa nguvu ya fedha ya bosi wa GSM na nikaongea nao na tukakubaliana sikuweza kuacha hizo fedha. Ila niliona pia Yanga ni sehemu nzuri kuja kufanya kazi,” alisema.

ANAVYOIONA YANGA

Anasema tangu alipotua Yanga hadi sasa anasikia ni timu kubwa Afrika, kitu kinachompa furaha ya kuitumikia kwa mkataba wa miaka miwili na baada ya kwisha atajua nini afanye.

“Tangu nikiwa mtoto nimekuwa naisikia Yanga maana mababu, baba na kaka zetu wameichezea. Hivyo najivunia kuwa sehemu ya timu kwa wakati wangu. Nitapambana ili kuacha alama ya kukumbukwa, kuna wachezaji wa kutoka Congo wamecheza hapa kwa mafanikio nami nataka kupita huko.”

MAKOMBE YANAKUJA

Moloko anasema anatambua Yanga haijachukua mataji muda mrefu, ndio maana imesajili mastaa kama Khalid Aucho, Shaban Djuma, Fiston Mayele, Diarra Djigui na kurejeshwa kwa Heritier Makambo na wengine waliopo akiwamo yeye lengo likiwa ni kufanikisha hilo.

Anasema kwa namna kikosi chao kilivyo ana uhakika msimu huu kitakomba mataji ya kutosha, ikiwamo ya Ligi Kuu Bara na hata Kombe la ASFC - muhimu soka liachwe lichezwe uwanjani.

“Ndio maana tumeanza kuchukua Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba ambayo ina ushindani mkali. Hilo linatupa nguvu ya kupambana kuamini hakuna linaloshindikana. Kila mchezaji ana hamu kuona taji la msimu huu tunalichukua na sioni kama Yanga hii itashindwa kuwa bingwa msimu huu,” anasema.

PRESHA YA TUISILA

Moloko amesajiliwa Yanga kama mbadala ya winga aliyekuwa na mbio, Kisinda, aliyeuzwa Morocco na akiulizwa anawezaje akaziba pengo la staa huyo aliyewadatisha Wanayanga, jibu lake ni jepesi tu.

“Kisinda alifanya kazi yake akaondoka, nitafanya kazi yangu kwani ndani ya miaka miwili niliyosaini mkataba nimejipanga kuhakikisha huduma yangu inakuwa muhimu kwa timu

najua kwamba watu wanataka kazi kubwa kama Kisinda aliyoifanya, nafikiri watafurahia kazi yangu pia,” anasema.

Mbali na hilo, anasema Ligi Kuu Bara ni ngumu kwani kila timu ina ushindani unaoonyesha malengo, jambo analoliona ni zuri litakalomfanya mchezaji kujituma kwa bidii.

“Japo hadi sasa ukiondoa Yanga timu ninazozijua ni Simba, Azam na Namungo, kwani ndizo nilizocheza nazo na nyingine nimeziona. Kupitia mechi hizo nimeona mpira si mwepesi na ni wa nguvu,” anasema

KUMBE NI BEKI

Moloko aliyefunga bao moja katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara anafichua kuwa kabla ya kuanza kucheza kama winga alianzia beki namba mbili, lakini alibadilishwa na kocha Shiko Mukiba wa timu ya Rangers inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu nchini DR Congo.

“Maisha yangu ya soka sikuanzia kucheza kama winga. Huko nyuma nilikuwa nacheza kama beki wa kulia, huyo kocha aliniambia nitakuwa mzuri zaidi nikicheza kama winga, aliona hivyo baada ya kuwa beki mzuri ninayepandisha mashambulizi na kurudi kukaba. Tangu hapo nimekuwa nikicheza nafasi hiyo hadi sasa, ila nina uwezo mkubwa kucheza beki ya pembeni upande wa kulia.”

AICHAMBUA SIMBA

Moloko alikuwa staa muhimu wakati Yanga inaifunga Simba kwa 1-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii, kwani alikuwa mmoja wa wachezaji waliompa wakati mgumu beki wa kushoto wa Wekundu wa Msimbazi, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Staaa huyo ameichambua Simba na kusema kung’ara kwake siku ya Ngao ya Jamii ilichangiwa na kutokuwa mgeni wa kucheza dabi, kwani amecheza nyingi na timu kubwa, hivyo haikuwa ngumu kwake kuikabili Simba kuhakikisha anatoa huduma inayoisaidia timu yake kupata ushindi.

“Nilipocheza mechi ya Simba hapa wala sikuwa na presha, hizi mechi nimecheza sana na nikafanya vizuri. Sikutaka kuingia presha hata kidogo ambayo labda ingenifanya nishindwe kufanya vizuri,” anasema.

“Lakini Simba nao nilikuwa nawajua kitu ambacho nilijipanga ni kuhakikisha napandisha mashambulizi na kuja kusaidia kukaba kama ambavyo kocha alikuwa anataka. Nashukuru mwisho wa siku tukafanikiwa kushinda mechi kubwa.”

Kuhusu kikosi cha Simba, Moloko anasema kwa tathmini yake na jinsi alivyoiona Simba nyuma ni wazi imepungua nguvu kubwa kulinganisha na ilivyokuwa misimu miwili iliyopita na kusisitiza kwua imechangiwa kwa kiasi kikubwa kuondoka kwa Clatous Chama na Luis Miquissone.

Hata hivyo, anasema licha ya kuondoka kwa nyota hao wawili, lakini bado Simba hawezi kusema ni mbovu kwani wachezaji walionao wakizoeana wanaweza kusumbua katika ligi.

“Sio mara ya kwanza kucheza na Simba, nimekutana nao Ligi ya Mabingwa Afrika. Ile tuliyoifunga mabao 5-0 kabla ya kulipa kiasi tuliporudiana nao hata Tanzania na kisha ikatufunga tena msimu uliopita, kwa jinsi nilivyoiona Simba ya msimu uliopita ilikuwa bora zaidi kushinda hata ile ya wakati tunawafunga 5-0. Na kwa kikosi cha msimu huu kimepungua nguvu kidogo inawezekana ni kutokana na kuondoka kwa Chama na Miquissone, ila sio kama wana timu mbovu wana wachezaji wazuri lakini wanahitaji muda kukaa sawa tena wasiwe na haraka,” anasema.

MAKALI KAMA WINGA

Kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi anataka kuona safu ya ushambuliaji inacheza kwa ushirikiano na hapa Moloko anaeleza anachotaka kufanya akicheza kama winga.

“Sina tatizo katika kutoa pasi ya kufunga. Hiyo ndio kazi yangu ya kwanza. Kocha yupo sahihi hakuna kitu bora kama kucheza kwa ushirikiano, ila zipo nafasi ambazo kama njitaona naweza kufunga nitafunga mfano kama hii ambayo niliipata katika mechi dhidi ya Geita Gold hakukuwa na ulazima wa kuanza kuangalia nani atafunga wakati mashabiki wanaona kabisa naweza kufunga. Ikija kama vile nitafunga sana,” anasema.

“Ujue kutoa pasi kwangu huwa naangalia namna mchezaji alivyo tayari kuifanyia kazi nikimpa, na sio kutoa kwani wakati mwingine unaweza kuipunguzia timu mabao kizembe.”

CHUMA CHA RELI

Moloko ni kati ya wachezaji wenye miili midogo, lakini anasema asichukuliwe poa kwani ni kama chuma cha reli.

Winga huyo anawatoa hofu mashabiki wa Yanga akisema kama ilivyo reli ni nyembamba, lakini inabeba treni yenye uzito mkubwa kwa vile yeye ni mwanasoka na amekuwa akijifua mazoezini vya kutosha ili kumrahisishia kazi zake uwanjani na kusisitiza atazidi kuwafurahisha katika ligi.

“Soka ni akili na mbinu na sio mabavu. Nitajitahidi kutumia uwezo wangu kwa mbinu kali kuhakikisha nawapa raha mashabiki wangu na kuisaidia timu kupata ushindi,” anasema Moloko huku mshambuliaji Fiston Mayele akicheka akimtania kwamba anatakiwa ale sana chakula.

KISWAHILI TATIZO

Moloko anasema kama kuna changamoto ngumu kwake ni kutojua Kiswahili na kujikuta anapata wakati mgumu kuzungumza na wachezaji wenzake kambini.

“Kuna wakati mwingine natamani kuwaambia kitu nashindwa. Natamani kucheka nao ila siwezi kuzungumza Kiswahili. Najua kidogo kama ‘mambo, poa’, ‘mzima’, hivyo tu ila nitaendelea kuzoea najifunza nafikiri nitajua na kuondokana na changamoto hiyo,” anasema.

JINA LA JESUS

Ukiachana na mshambuliaji wa Manchester City, Mbrazil Gabriel Jesus (24) aliyemzidi miezi saba Jesus wa Yanga, ndani ya jina hilo kuna siri nzito.

Baada ya Yanga kumsajili Moloko ambaye jina lake la kwanza (Jesus), lilionekana kuwastajaabisha wadau wa soka nchini na hapa anafichua.

“Nilipewa jina hilo, kwa vile nilizaliwa Desemba 25, 1997 ikiwa ni Sikukuu ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Kupitia jina hilo nimefanikiwa sana ingawa siwezi kuweka wazi kwamba ni kitu gani,” anasema Moloko ambaye majina yake kamili ni Jesus Ducapel Ito Moloko.

Anapoulizwa anajisikiaje pale anapoanguka uwanjani, mashabiki kutania “nyanyuka kwani Yesu hawezi kusaidiwa”, anajibu kuwa anatambua hilo, ila mashabiki wanapaswa kufahamu anajipigania mwenyewe katika mafanikio yake.

“Sisi katika imani yetu tunaamini Yesu Kristo baada ya kupigiliwa msalabani alikufa, kisha akajifufua mwenyewe siku ya tatu. Ndio maana nasema hilo jina limenifanyia mengi sana ambayo siwezi kuyaweka wazi, watu wasilichukulie poa,” anasema.