Dili la N’Diaye laingia mdudu, Mbrazil kutua Simba

MABOSI wa Simba bado wanazidi kukuna kichwa juu ya mchakato wa kusaka kocha mpya, baada ya kubainika ni ngumu kumleta nchini Msenegal, Lamine N’Diaye kutokana na dili hilo kuingia mdudu na sasa wameelekeza nguvu kwa majina matatu, likiwamo lile la kocha aliyetakiwa na Yanga.

Mwishoni mwa wiki iliyopita mmoja wa vigogo wa Simba alikaririwa kwamba kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023 wangemleta kocha mwenye asili ya Afrika ambaye ilibainika ni N’Diaye aliyepo AC Horoya ya Guinea, lakini mipango hiyo imekufa na sasa wamegeukia wengine.

Habari za kuamini kutoka ndani ya Simba, zinasema Waguinea waliposikia dili hilo la kocha huyo kutakiwa na Simba wameamua kukaza kwa kuweka mzigo mkubwa, wakilenga kumzuia asiondoke wakati wakijiandaa na mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikipangwa sambamba na Simba.

Kocha huyo wa zamani wa AC Leopards ya Congo Brazzaville, TP Mazembe ya DR Congo na Al Hilal ya Sudan, ana mkataba na klabu yake ya Horoya aliyojiunga nayo mwaka 2019 na Simba ilitaka kuununua ili iwe naye tangu kabla hajaletwa Zoran Maki aliyekaa Msimbazi kwa muda mfupi kisha kutimkia Al Ittihad ya Misri.

Japo imefichwa kiwango cha fedha kilichotakiwa, lakini inadaiwa dau kubwa la kuununua mkataba ndio lililoifanya Simba kuachana naye na sasa kuwageukia makocha wengine akiwamo yule aliyekuwa akitakiwa na Yanga wakati wa vuguvugu la kutaka kutemwa kwa Nasreddine Nabi.

Mwanaspoti limepenyezewa jana kwamba mmoja ya mabosi wa Simba alifanya kikao kwa njia ya mtandao na makocha watatu kwa ajili ya kufanya usaili wa mmoja kutua kabla timu haijaenda Zanzibar kwenye michuano ya Mapinduzi.

Hata hivyo, licha ya kutotajwa majina ya makocha hao, lakini Mwanaspoti limejiridhisha moja ya majina hayo ni la kocha wa Vipers ya Uganda, Robertinho Oliviera aliyewahi kutakiwa na Yanga ambaye tangu awali alishazungumza na mabosi wa klabu hiyo kupitia Mtendaji Mkuu anayemaliza muda, Barbara Gonzalez.

Tayari kocha huyo ameshaaga Vipers kwa makubaliano ya pande zote mbili na klabu hiyo imetoa taarifa, ingawa haijaainisha anaenda wapi, lakini Mwanaspoti linafahamu atatua muda wowote kuanzia leo akiwa na msaidizi wake tayari kumalizana na kuanza kazi Msimbazi.

Kwa mujibu wa chanzo hicho kuna uwezekano mkubwa kwa Mbrazili huyo wa Vipers, yaani Robertinho akawa kwenye nafasi nzuri ya kulamba dili hilo la Simba na kuja kuanza kazi kabla ya Mapinduzi Cup inayoanza Januari 1-13.

Kama mambo muhimu ikiwemo yale ya maslahi yataenda tofauti labda dili la Robertinho ndio linaweza lisikamilike na bosi huyo wa Simba akaenda kufanya uamuzi mwingine ila hadi sasa nafasi kubwa ya kukinoa kikosi hicho ipo kwake.


MSIKIE ROBERTINHO

Alipotafutwa Robertinho alisema kuna mawasiliano mazuri kati yake na kiongozi wa Simba (jina lake tunalo) na amewaeleza kila kitu cha msingi anachohitaji ili aje kuifundisha timu hiyo kama ilivyokuwa wakati wa mkutano huo wa mtandaoni.

“Kwa upande wangu nilifanya hiyo zoom meeting vizuri kabisa nadhani imebaki wao tu kuamua.”