Dalali: Ilibaki kidogo ning'atwe na chatu kisa Simba

SIMBA Day ya mwaka huu itafanyika mara ya 13 tangu ilipoanzishwa 2009 chini ya aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali ambaye anasimulia alivyokaribia kung’atwa na chatu kwa sababu ya Wekundu, huku mastaa wa zamani wakitaka apewe tuzo ya heshima.

Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ aliyekuwa mshambuliaji nyota wa timu hiyo, amesema ipo haja viongozi wa sasa wanaoliendeleza tamasha hilo wamuenzi Dalali akiwa hai kutokana na misingi aliyoiweka. “Viongozi walioanzisha tamasha hilo ambao wapo hai wakiongozwa na Dalali. Ni vyema awamu hii wakumbukwe ili wajisikie faraja kuona walifanya jambo linaloendelea kuleta neema kwenye timu, angalau wapewe hata tuzo,” alisema.

Naye kocha mkongwe Abdallah Kibadeni alisema ndani ya Simba kuna wazee waliovuja jasho kwa ajili ya timu hivyo aliomba wapewe heshima wakiwa hai.

“Laiti soka lingekuwa kwenye mfumo wa serikalini wenye umri kama wangu wangekuwa wanakula pensheni ya jasho lao, ila huku kwenye soka haipo hivyo. Ndio maana nasema hilo tamasha lazima litambue wazee ambao waliweka misingi inayoendelezwa kwa sasa,” alisema.

Alipoulizwa Dalali (pichani) ni kitu gani anakikumbuka tangu alipoanzisha Simba Day 2009, alijibu: “Nakumbuka mwaka 2007 wakati tumekwenda kutembelea uwanja wa Bunju mimi na Mwina Kaduguda wakati huo akiwa katibu wangu nilinusurika kung’atwa na chatu, maana lengo la hilo tamasha lilikuwa ni huo uwanja.”

Alieleza kuwa wakati anakagua uwanja sehemu alipokuwa amesimama alipita chatu mkubwa anatoka vichakani na kwenda kwenye mbuyu. “Kuna mama mmoja alimuona akaniita wee baba kuna mdudu anapita pembeni yako simama bila kujitingisha, nikafanya hivyo akapita na kuingia kwenye mbuyu ilikuwa siku nzito sana kwangu, lakini yote hayo ilikuwa ni kupigania Simba iwe na mafanikio,” alisema Dalali.

“Ule mbuyu upo hadi leo. Baada ya yule chatu kupita nikamfuata yule mama akaniambia ni kawaida ya huyo chatu kupita saa sita mchana na kuingia kwenye mbuyu kisha saa tisa 9:00 jioni kurejea alikotoka. Kiukweli nashangaa hadi leo namna Mungu alivyoniepusha ndio maana nipo hai.”

Anachotamani kukiona katika tamasha la mwaka huu ni uongozi kuleta timu inayoendana na Simba ambayo ina thamani kubwa kimataifa akishauri ikiwezekana wacheze na Wydad Casablanca ya Morocco.