Coastal, Polisi Tanzania vitani leo

MCHAKAMCHAKA wa Ligi Kuu Bara utaendelea leo katika viwanja viwili ambapo timu nne zitakuwa zikipambana kutafuta alama tatu muhimu za kuwaweka salama kabla ya ligi kumalizika.

Saa 8:00 mchana pale Tanga kwenye dimba la Mkwakwani kutakuwa kunapigwa mechi kali kati ya wenyeji Coastal Union na Polisi Tanzania.

Mechi hii inatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake kulingana na tofauti ya pengo la alama kwa timu hizo. Coastal ipo nafasi ya 13 baada ya kucheza mechi 28 na alama 33 huku Polisi wakiwa nafasi ya sita na alama 38 walizovuna kwenye mechi 29 walizocheza.

Coastal itahitaji alama tatu ili kufikisha 36, pointi mbili nyuma ya Polisi na kusogea hadi nafasi ya 11 baada ya mechi 29 huku Polisi ikiingia kutafuta alama tatu zitakazoisogeza hadi nafasi ya tano.

Mechi nyingine ya leo itapigwa kwenye uwanja wa Karume Mara ambapo vita ya alama tatu inatarajiwa kuwa kubwa zaidi.

Wenyeji Biashara wapo nafasi ya nne na pointi 44 huku Dodoma wakiwa nafasi ya saba na alama 38. Timu zote mbili zimecheza mechi 28.

Kwa mara ya mwisho timu hizi zilipokutana Novemba 20 mwaka jana Dodoma wakiwa wenyeji mechi iliisha kwa sare ya bao 1-1.