Cioaba awashangaa viongozi wa Azam

Friday November 27 2020
cioba pic

VIPIGO viwili mfululizo ambavyo wamekutana navyo matajiri wa Ligi Kuu Bara, Azam FC dhidi ya KMC na Yanga ndivyo vinavyodaiwa kuwa ni chanzo cha kutimuliwa kwa kocha wao Aristica Cioaba raia wa Romania huku akionekana kushangazwa na uamuzi huo.

Mbali na mechi hizo mbili mfululizo, Azam walipoteza dhidi ya Mtibwa Sugar walitoka sare na JKT Tanzania.

Jana Alhamis Novemba 26, 2020, uongozi wa Azam FC ulitangaza kuachana na kocha huyo ambapo sasa timu itakuwa chini ya kocha msaidizi Bahati

Katika taarifa hiyo, uongozi wa Azam FC ulisema umeachana na kocha huyo baada ya kukaa na kujadiliana pande zote mbili, uongozi na kocha wao.

Azam msimu huu walianza ligi kwa kishindo walishinda michezo saba mfululizo huku wakiwa na matumaini makubwa ya kuwa kwenye ushindani mkubwa wa kuwania ubingwa wa ligi.

Akizungumza na Mwanaspoti Online, Cioaba amesema mara baada ya mechi na Yanga kumalizika siku iliyofuata alipokea simu kutoka kwa kiongozi wa juu wa Azam ambaye aliomba kukutana naye ili kufanya kikao kuhusu mwenendo wa timu hiyo.

Advertisement

"Nashangaa mara baada ya kukutana naye aliniambia wanasitisha mkataba wangu na watanipa stahiki zangu zote na sababu kubwa ya wao kufikia hivyo ni mwenendo mbaya wa timu,

"Baada ya kuniambia hivyo niliwauliza mwenendo mbaya wa timu ni upi kwani tumekusanya pointi 25, katika michezo 12 tukiwa nyuma kwa pointi tatu na vinara wa ligi Yanga hakunipa majibu ya kueleweka mwisho wa mazungumzo aliniambia huo ndio uamuzi waliofikia.

"Ili timu yoyote ifanikiwe si Azam tu bali nyinginezo lazima wote muwe na mlengo wa kuangalia malengo yenu na kila mmoja kupambana kwa nafasi yake ili kutimiza hilo lakini wasiwepo wengine ambao katikati ya hilo wanakuwa na mahitaji yao mengine binafsi hakutakuwa na mafanikio tena," amesema na kuongeza, 

"Nashukuru kamati ya tuzo kutambua ubora ambao nimeonyesha hasa katika kupata matokeo mazuri mfululizo na kunipatia zawadi mara mbili mfululizo, waajiri wangu hawakuliona hilo na wameamua kufikia maamuzi ya kuniondoa hapa," amesema Cioaba

Pia amewapongeza mashabiki kwa kuipa nguvu timu hiyo inapocheza mechi zao zote; "Niwapongeze mashabiki na wale wote ambao walikuwa wanaipa nguvu Azam kwa muda ambao nimefanya kazi hapa na kufanikiwa kukipata hicho nilikuwa na malengo makubwa ya kufanya zaidi ila hilo limeshindikana,".

Azam mpaka wanaachana na Cioaba wapo nafasi ya pili wamecheza michezo 12, wameshinda saba, wametoka sare moja, wamefungwa mitatu, wamefunga mabao 18, wamefungwa mabao sita, wamebaki na pointi 25.

Na THOBIAS SEBASTIAN

Advertisement