Chama ni fundi, halafu mtu wa zali

CLATOUS Chama ni fundi wa mpira nyie acheni, halafu sasa kama hujui jamaa lina bahati kinoma hasa zinapokuja mechi za kuamua matokeo kwa timu yake ya Simba.

Licha ya juzi kuwaudhio baadhi ya mashabiki wa kuonekana kuupozesha mchezo kila alipokuwa na mpira, lakini ndiye aliyeamua matokeo ya mchezo huo kwa kufunga bao la pili na la nne lililoivusha Simba robo fainali kibabe mbele ya As Vita ya DR Congo.

KWA kufunga bao la mwisho dhidi ya Vita katika ushindi wa mabao 4-1 juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, imemfanya Chama aendeleza rekodi yake ya kufunga mabao ya mwisho katika mechi ya kuihakikishia Simba kufuzu hatua nyingine katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hii ni mara ya tano kwa Chama kufanya kitu kama hicho tangu alipojiunga na Simba mwaka 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia, ambapo amekuwa akifunga mabao yanayogongelea msumari wa mwisho katika jeneza la wapinzani wa Simba na kuhitimisha ndoto zao za kusonga mbele katika mashindano hayo.

Nyota hiyo ya jaha kwa Chama ilianzia Novemba 28, 2018 pale alipoifungia Simba bao la mwisho dhidi ya Mbabane Swallows ya Eswatini katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya mashindano hayo uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini ambao waliibuka na ushindi wa mabao 4-1.

Ushindi huo wa Simba nyumbani uliiweka Simba katika nafasi nzuri ya kufuzu raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/2019 ambapo walikwenda ugenini huko Mbabane, Eswatini ambako waliibuka na ushindi wa mabao 4-0 ingawa Chama licha ya kupachika mabao mawili, bao la mwisho lilifungwa na Meddie Kagere.

Bahati hiyo kwa Chama ilijirudia Disemba 23, 2018 pale alipofunga bao la tatu katika mechi dhidi ya Nkana iliyochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao ulikuwa wa marudiano wa hatua ya kwanza na kuifanya Simba iibuke na ushindi wa mabao 3-1 uliowapeleka hatua ya makundi ya mashindano hayo msimu huo.

Machi 16, 2019, Chama alifunga bao la mwisho katika ushindi wa mabao 2-1 ambao Simba waliupata dhidi ya AS Vita ambalo liliivusha Simba na kuipeleka katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo msimu huo wa 2018/2019.

Nyota ya Chama iliendelea kung’aa tena Novemba 29, 2020 ambapo alifunga bao pekee la ugenini dhidi ya Plateau ya Nigeria lililoivusha Simba kutinga raundi ya kwanza kwani katika mechi ya marudiano jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.

Chama tena alikua kurudia balaa lake Januaria 6 mwaka huu alipofunga hesabu kwenye mechi dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe katika ushindi wa mabao 4-0 ilioupata katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo alipachika bao la nne kwa mkwaju wa penati iliyopatikana baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa faulo ndani ya eneo la hatari la wapinzani wao.

Na juzi tena dhidi ya Vita, Chama aliyepachika mabao mawili akifunga la pili na lile la mwisho katika dakika ya 84 akimalizia kwa ustadi pasi ya Luis Miquissone.

Kocha wa Simba Queens, Musa Hassan ‘Mgosi’ alisema kinachombeba Chama ni akili yake inayofanya kazi kwa haraka pindi anapokuwa uwanjani.