Chama azidi kutakata Afrika

Chama azidi kutakata Afrika

Muktasari:

  • KIUNGO nyota wa Simba,Clatous Chama amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa wiki ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika mzunguko wa tano.

KIUNGO nyota wa Simba, Clatous Chama amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa wiki ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika mzunguko wa tano.

Chama alihusika katika mabao matatu kati ya manne ambayo Simba ilifunga kwenye mchezo dhidi ya  AS Vita uliofanyika Aprili 3 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika mchezo  huo ambao Simba ilifunga mabao 4-1, Chama alifunga  mabao  mawili na kutoa pasi  moja ya bao  hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa timu yake kufuzu kwenye  robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Baada ya kuonesha kiwango bora katika mchezo huo, Chama aliingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania tuzo ya mchezaji bora wa wiki inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika(Caf) na kuibuka  mshindi kwa kuwashinda Amir Sayoud wa CR Belouizdad, Ricardo Goss wa Mamelodi Sundowns na Ferjani Sassi wa Zamalek.

Hii inakuwa mara ya pili katika msimu huu kwa klabu ya Simba kutoa mchezaji bora wa wiki kwani hapo awali katika raundi ya pili ya michuano Luis Miquissone alichaguliwa mchezaji bora  wa wiki.

Sambamba na hilo, pia Chama na Miquissone  wametajwa kwenye kikosi bora cha wiki kutokana na kiwango bora walichokionesha kwenye mchezo dhidi ya AS Vita.