Chama aongeza mzuka Simba

Monday June 21 2021
chama pic
By Thobias Sebastian

BAADA ya kuwa nje kwa takribani wiki tatu kiungo wa Simba amerejea kikosini na kuanza mazoezi na wenzake kujiandaa na mechi dhidi ya Mbeya City.

Mwanaspoti ilitia timu katika Uwanja wa Mo Simba Arena ambapo nyota hao wanafanya mazoezi leo Jumatatu Juni 21 na kumkuta Chama ambaye alifiwa na mke wake wakati timu hiyo ilipokuwa Ruangwa mkoani Lindi kucheza dhidi ya Namungo akifanya mazoezi.

Kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa wa kufanya vitu bora anapokuwa na mpira aliwasili nchini Jumapili usiku na Jumatatu kuamkia katika mazoezi ya timu hiyo.

Chama alianza kufanya mazoezi mepesi na wenzake lakini baadae kocha wa viungo, Adel Zrane alimchukua na kwenda nae pembeni kufanya mazoezi yao binafsi.

Wakati huo huo, kocha wa Simba, Didier Gomes alisema wachezaji, viongozi na benchi la ufundi wote wamefurahishwa na urejea wa Chama tena akiwa fiti na utimamu wa mwili.

“Ni jambo la furaha Chama kujiunga nasi kwa mara nyingine tena baada ya matatizo, amerejea akiwa fiti na jukumu limebaki kwangu kama naweza kumtumia katika mechi ya leo dhidi ya Mbeya City,” alisema Gomes na kuongezea;

Advertisement

“Chama anaweza kutumika kwani ni mchezaji muhimu lakini mchezo huo wa Mbeya City unaweza ukawa sehemu kwake ya kumuandaa na mchezo mgumu wa nusu fainali ya kombe la shirikisho (ASFC), dhidi ya Azam pamoja na ule wa Yanga ambao tumepanga kutangaza ubingwa dhidi yao.”

Advertisement