Bonasi Simba sasa zipo hivi, Try Again afunguka

HIVI karibuni tajiri wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’ alijiuzulu uenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Salim Abdallah ‘Try Again’ kuteuliwa kushika nafasi hiyo kitu ambacho kilizua mjadala huku ukienda mbali zaidi kwamba huenda hata zile bonasi kwa wachezaji zikaondolewa, lakini hilo limefafanuliwa.

Mwanaspoti linafahamu kuwa, nyota wa Simba msimu uliopita walikuwa wakipewa bonasi nono kwenye mechi za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika ambako sasa wanaanza kutupa karata ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy FC ya Botswana Oktoba 15 na mshindi wa mechi zote mbili atafuzu hatua ya makundi.

Bonasi hizo zilikuwa kati ya Sh200 milioni, Sh300 milioni na Sh150 milioni kwa kutegemea na matokeo, timu ikishinda au kutoka sare walizokuwa wanagawana.

Akizungumza na Mwanaspoti, Try Again alifafanua juu ya mipango na mikakati yao kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika.

“Wanasimba wasiwe na wasiwasi, kila kitu kitaenda sawa kama ilivyokuwa hapo nyuma, hakuna kitakachobadilika, Mo yupo Simba hadi sasa japokuwa katoka nafasi hiyo lakini yupoyupo sana tu,” alisema Try Again.

Kuhusu matokeo ya mechi mbili za Ligi Kuu Bara, ambazo Simba ilitoka suluhu na Biashara, kisha ikapata ushindi kiduchu kwa Dodoma Jiji wa bao 1-0, Try Again alisema: “Ligi Kuu mpira unachezwa kwa nguvu na kukamiana, lakini Ligi ya Mabingwa timu zinacheza kwa utulivu na mpira unapigwa. hHivyo Wanasimba msiwe na wasiwasi Simba yenu ipo na ni nzuri tu.”


WADAU NAO

Mchezaji wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema alichokifanya Mo ni jambo la kawaida kama kiongozi, lakini kutoka kwake sio sababu ya kushindwa kuendelea kujitolea.

“Mo ni Simba yule. Hata kama katoka lakini ataendelea kusapoti kama nyuma ili kuhakikisha timu inafikia malengo ambayo anatamani kuyaona,” alisema.

Kenny Mwaisabula alisema: “Try Again hata hiyo nafasi aliyonayo ya mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi naamini atakuwa anafanya kazi kwa ukaribu sana na Mo, hivyo kila kitu kitaenda sawa tu kama ilivyokuwa.”