Bocco, Mkude wakabidhiwa Mbeya City, Kanoute nje

Mbeya. Baada ya kufanya kweli katika mechi iliyopita, leo tena nahodha na straika wa Simba John Bocco amekabidhiwa jukumu 'kuimaliza' Mbeya City, huku Sadio Kanoute akitolewa kwenye kikosi kinachoanza hata wale wa benchi.

Bocco akicheza mechi yake ya kwanza msimu huu, alionesha soka safi hadi kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Ruvu Shooting.

Katika ushindi huo, staa huyo wa kimataifa, aliweka kambani mabao matatu 'hatitriki' na kuwa mchezaji wa pili kufunga idadi hiyo ya mabao katika mechi moja akitangulia staa wa Yanga, Fiston Mayele.

Hata hivyo Bocco aliyewahi kung'ara na Azam FC ndiye mchezaji ambaye ameifunga sana Mbeya City pindi wanapokutana bila kujali nyumbani au ugenini, akiwa amefunga 13 kati ya 29 timu yake iliyofunga dhidi ya City katika mechi 14 walizokutana tangu msimu wa 2014/15.

Katika kikosi kinachoanza leo, kocha mkuu wa Simba, Juma Mgunda amefanya badiliko la mchezaji mmoja, Kanoute ambaye nafasi yake amesimama Jonas Mkude.


Kikosi hiki hapa;
Aisha Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Husein, Joash Onyango, Henock Inonga, Jonas Mkude, Clatous Chama, Mzamiru Yassin, John Bocco, Moses Phiri na Nelson Ocrah.

Wanaosubiri benchi ni Beno Kakolanya, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Mohamed Ouatara, Akpan, Pape Sakho, Habibu Kyombo na Kibu Denis.