Bocco amdatisha Nabi, Fei Toto amvuruga Gomes

Monday July 19 2021
boko pic
By Clezencia Tryphone

LICHA ya Simba kuwa na wachezaji wengi wazuri, mziki mnene wa nahodha wake, John Bocco umemtingisha Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema mshambuliaji huyo ngongoti ni moja ya wanaomuumiza kichwa kabla ya fainali ya Kombe la ASFC, huku Didier Gomes akimtaja Fei Toto.

Nabi alimwagia sifa Bocco akidai kuwa ni mmoja ya washambuliaji hatari aliowaona kwenye Ligi Kuu Bara na kusema kama mabeki wakizembea kidogo kumchunga huwa ni rahisi kuwatia maumivu, wakati Gomes alisema anamkubali Feisal Salum kwa kipaji alichonacho.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huiyo mwenye uraia pacha wa nchi za Tunisia na Ubelgiji, alisema Bocco anajua kutumia nafasi anazozipata akiwa uwanjani hivyo anamuelewa sana.

Nabi alisema straika amemuweka kuwa kipaumbele cha kuchungwa zaidi uwanjani katika mchezo wao wa Jumapili mjini Kigoma, akitumia mbinu zilezile walizomdhibiti kwenye Kariakoo Derby ya Ligi Kuu Bara ilipopigwa Julai 3 na Simba kulala 1-0 kwa bao la Zawadi Mauya.

“Simba ina wachezaji wengi wazuri lakini Bocco ndiye hatari zaidi, napenda aina yake ya uchezaji, kwani anajua nini akifanye katika wakati sahihi, anajitahidi sana kutumia nafasi. Hata akiwa mbele peke yake anapambana kupata nafasi ya kufunga. Ni mchezaji wa kuchungwa zaidi uwanjani.”

“Hata Luis (Miquissone) Chama (Clatous) nao ni wazuri, lakini Bocco ni balaa zaidi, kwani pia hutumia urefu wake na ni mtu wa kuchungwa sana timu zetu zitkazpokutana,” alisema Nabi.

Advertisement

Wakati Nabi akikubali uwezo wa Bocco, upande wa Didier Gomes wa Simba alikaririwa hivi karibuni kuwa anavutiwa na kiungo wa Yanga, Feisal Salum ’Fei Toto’ kutokana na uwezo mkubwa wa mchezaji huyo.

“Feisal ni mchezaji mzuri sana pale Yanga. Anajua mpira, anajua namna gani ya kuwasoma wapinzani na kupeleka mashambulizi mbele, nampenda sana,” alisema Gomes.

Simba na Yanga zinakutana Jumapili kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), ikiwa ni wiki tatu tangu zikutane katika Ligi Kuu Bara jijini Dar es Salaam na Yanga kushinda 1-0.

Mechi hiyo ya kulinda heshima baina ya timu hizo kwa kuzingatia tayari zimeshakata tiketi ya michuano ya kimataifa, kwa Simba ni muhimu ili kulipa kisasi na watani wao kubeba taji lao la kwanza katika misimu ya soka la Tanzania Bara .

Advertisement