Bigirimana sasa kulipwa kwa mafungu

ALIYEKUWA kiungo wa Yanga, Mrundi Gael Bigirimana amekubali yaishe na sasa anajiandaa kuvuta mkwanja wa kutosha kutoka kwa klabu hiyo baada ya kukiukwa kwa vipengele vya mkataba baina yao, lakini ikielezwa atalipwa kwa awamu tofauti na sio kwa mkupuo.

Yanga ilimchomoa Gael kikosini dakika chache kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa Januari 15 na nafasi yake kuchukuliwa na beki kutoka Mali, Mamadou Doumbia lakini staa huyo amewaganda Wanajangwani hao akitaka wamlipe stahiki zake na fidia haraka iwezekanavyo ili aendelee na yake.

Mwanzo Yanga ilitaka Gael aendelee kuwa ndani ya kikosi ili acheze Kombe la Shirikisho Afrika lakini sio Ligi baada ya wachezaji 12 wa kigeni kutimia, lakini nyota huyo amegomea jambo hilo.

Gael alisajiliwa Yanga mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili, lakini hakuonyesha ubora ambao Wanajangwani hao waliutarajia kutoka kwake jambo lililofanya waachane naye baada ya miezi sita tu na Mwanaspoti limepenyezewa timu hiyo inatahitajika kumlipa kiungo huyo Dola 300,000 (karibu Sh700 milioni).

“Ilikuwa lazima wamlipe, meneja wake alikuja kutokea England kuonana na uongozi na wamekubali kumlipa kwa mafungu,” chanzo chetu kilieleza.