Biashara yaitangulia Simba Uwanjani

TIMU ya Biashara United ndiyo imekuwa ya kwanza kuwasili katika Uwanja wa Karume, Musoma kwaajili ya maandalizi ya mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Simba.

Biashara ambao ni wenyeji wa mechi hiyo wameingia uwanjani hapo saa 8:20 mchana kwa usafiri wa basi lililokwenda hadi kwenye mlango wa vyumba vya kubadilushia nguo na wachezaji sambamba na viongozi wa benchi la ufundi kushuka na kuingia ndani.

Wakati wachezaji wa Biashara wakishuka, mashabiki waliopo wa timu hiyo waliopo uwanjani hapo walionekana kuwashangilia kwa shangwe kubwa sana.

Saa 8:37, Simba nao waliingia uwanjani hapo na gari aina ya Coaster nyeupe na kwenda hadi kwenye mlango wa kuingilia katika vyumba vya kubadilishia nguo.

Msafara wa Simba ulisindikizwa na magari mawili aina ya Noah yaliyokuwa yamebeba makocha na baadhi ya viongozi wa timu hiyo.

Kuingia kwa Simba kuliamsha shangwe la mashabiki wa timu hiyo uwanjani hapo huku wakimshangilia kila mchezaji na kiongozi wao.

Mtanange huo utaanza saa 10:00, kwenye Uwanja wa Karume, Musoma ambapo mashabiki wameingia ndani kwa viingilio vya  Sh 5000 kwa mzunguko na 20 elfu kwa VIP.