Beki Yanga asimulia dakika 90 za Biashara United

Muktasari:

  • KITASA wa Yanga, Dickson Job ameongelea dakika zake 90 za kwanza kucheza kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United kwa kusema zilikuwa za jasho na damu huku akieleza siri iliyomfanya kuaminiwa na kupewa nafasi.

KITASA wa Yanga, Dickson Job ameongelea dakika zake 90 za kwanza kucheza kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United kwa kusema zilikuwa za jasho na damu huku akieleza siri iliyomfanya kuaminiwa na kupewa nafasi.

Kwa mara ya kwanza tangu asajiliwe Yanga wakati wa dirisha dogo la usajili akitokea Mtibwa Sugar, Job alipewa nafasi ya kucheza chini ya kocha Juma Mwambusi kwenye mchezo huo wa Ligi ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Beki huyo wa kati mwenye miaka 20, alisema ile kusikia tu kwamba ataanza kwenye kikosi cha kwanza ambacho kitacheza dhidi ya Biashara, aliamini kuwa ule wakati ambao alikuwa akiupigania umewadia hivyo inampasa kuonyesha uwezo wake.

“Nilikuwa na matumaini kwamba ipo siku nitapata nafasi ila sikuwa najua kwamba ni kwenye mchezo dhidi ya Biashara, nilikuwa nikijituma sana mazoezini kwa sababu ndio sehemu ambayo niliona naweza kumshawishi mwalimu.

“Sikuwa na presha kwa sababu haikuwa mara yangu ya kwanza kucheza Ligi na kucheza na Ninja haukuwa mtihani kwangu kwa sababu ni kati ya wachezaji ambao nimekuwa nikielewana nao vizuri, sio yeye hata Lamine na Mwamnyeto,” alisema beki huyo.

Kuhusu mchezo ulivyokuwa, Job alisema ulikuwa mgumu na yote hiyo ilichangiwa na ubora wa Biashara, “Tumestahili kushinda kwa sababu tulikuwa bora zaidi yao, tulipambana kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu kitu ambacho naamini kimerejesha furaha kwa mashabiki wetu ambao walichukizwa na matokeo ya sare.”