Banda hadi mwakani

WINGA wa Simba, Peter Banda anatarajiwa kukaa nje ya uwanja hadi Februari 2023 akiuguza majeraha aliyoyapata kwenye mechi dhidi ya Singida Big Stars.

Banda aliumia kifundo cha mguu, 'Enka' kwenye mechi hiyo ya Ligi Kuu iliyopigwa Novemba 9 mwaka huu uwanja wa Liti mkoani Singida na kulazimika kutolewa nje katika kipindi cha pili dakika chache baada ya kuifungia Simba bao la kusawazisha akitokea benchi na mechi kumalizika kwa sare ya 1-1.

Staa huyo wa timu ya taifa ya Malawi, kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii, Twitter na Instagram amethibitisha hilo alipoweka picha yake na kuambatanisha maneno yaliyosomeka;

"Najisikia vizuri kiasi sasa kuliko mwanzo, baada ya majuma mawili nitarudi kumuona daktari kwa uangalizi lakini kulingana na majibu, nitakuwa nje kwa miezi mitatu," aliandika Banda na kuongeza;

"Naamini kwa baraka za mungu nitarudi tena uwanjani mwezi Februari,"

Banda tangu amejiunga na Simba akitokea Nyassa Big Bullets ya nchini kwao amekuwa akikumbwa na majeraha ya mara kwa mara jambo linalohatarisha nafasi yake ya kusalia ndani ya kikosi hicho.