Azam majanga, Dube avunjika

Azam majanga, Dube avunjika

Muktasari:

  • Dube raia wa Zimbabwe, aliumia dakika ya 15 kwa kuvunjika mfupa wa mbele wa mkono wake wa kushoto unaoitwa Ulnar, huu ni mfupa unaoanzia kwenye kiwiko na kushuka hadi kwenye kidole cha mwisho."

SAA chache tangu itoke kupokea kipigo kutoka kwa Yanga, Azam FC imepata pigo jingine baada ya kubainika straika wake tegemeo, Prince Dube amevunjika mkono, hivyo kukosa baadhi ya mechi za Ligi Kuu Bara ikiwamo ijayo ya ugenini dhidi ya Biashara United.
Dube alitolewa uwanjani dakika ya 18 kwa machela huku akionekana kuwa na maumivu makali wakati alipoanguka kwenye harakati za kuwania mpira kwenye Uwanja wa Azam Complex katika pambano la timu yake dhidi ya Yanga iliyowalaza bao 1-0.
Mara baada ya kutolewa na uwanjani alipewa huduma ya kwanza na kukimbizwa hospitalini kupata matibabu zaidi na imebainika amevunjika na uongozi wa klabu hiyo umepanga kumsafirisha Jumapili hii kwenda Afrika Kusini kwa matibabu ya kina.
Kupitia mitandao ya kijamii ya Azam iliandika; "
Dube raia wa Zimbabwe, aliumia dakika ya 15 kwa kuvunjika mfupa wa mbele wa mkono wake wa kushoto unaoitwa Ulnar, huu ni mfupa unaoanzia kwenye kiwiko na kushuka hadi kwenye kidole cha mwisho."
"Ataondoka nchini Jumapili ya Novemba 29, kwa shirika la ndege ya Kenya Airways (KQ), atatibiwa kwenye hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo Cape Town, chini ya daktari bingwa wa mifupa, Robert Nicolas," ilisomeka taarifa hiyo na kuongeza zaidi;

"Azam FC tumekuwa tukiitumia hospitali hii kutibia wachezaji wetu tangu mwaka 2011, tunampa pole na kumtakia matibabu mema na kupona haraka Dube."
Dube kabla ya kupata majeraha hayo ndio mfungaji bora wa kikosi cha Azam mpaka katika mzunguko wa 12, akiweka kambani mabao sita yaliyomfanya aongoze orodha hiyo ya ufungaji kwa muda mrefu kabla ya wiki iliyopita kupitwa na John Bocco wa Simba aliyefunga hat trick dhidi ya Coastal Union na kumfanya afikishe mabao saba, moja zaidi ya Mzimbabwe huyo.
Dube yupo sambamba na Adam Omar wa JKT Tanzania na kinda la Gwambina, Meshack Abraham kila mmoja akiwa na mabao sita mpaka sasa Ligi Kuu ikiwa inaingia raundi ya 13.

___________________________________________________________________

Na THOBIAS SEBASTIAN