Aucho aumia, kuikosa Namungo kesho

Aucho aumia, kuikosa Namungo kesho

Lindi. Yanga itamkosa kiungo wake mahiri Khalid Aucho katika mchezo dhidi ya Namungo kesho Novemba 20, baada ya kuumia kwa kupata mchubuko katika goti lake huku kocha wa timu hiyo Nasreddine Nabi akisema kuwa hana wasiwasi.

Yanga itakuwa ugenini kwenye uwanja wa Ilulu Lindi kuikabili Namungo ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Aucho amepata majeraha wakati akiitumikia timu yake yaTaifa ya Uganda ilipopambana na Mali Jumapili iliyopita.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema wamepata taarifa kutoka kwa daktari wa timu ya Taifa ya Uganda kuwa Aucho ameumia.

"Wametupa taarifa kuwa Aucho ameumia kidogo na atakaa nje ya Uwanja kwa siku nne hadi tano.

"Ni vizuri kuwa na mchezaji kama Aucho uwanjani kwani ana mbinu na akili lakini timu kubwa huwa haimtegemei mchezaji mmoja na ndio ilivyo Yanga wachezaji wote ni wazuri na naamini watapambana na kuipa timu matokeo kesho, amesema Nabi.

Pia Nabi amewashukuru wadhamimi wa Yanga, kampuni ya GSM kwa kufanikisha natibabu ya Mshambuliaji, Yacouba Sogne.

"Yacouba alikuwa Tunisia kwa matibabu na amerejea hivyo namuombea apone haraka na kurejea uwanjani kwani ni mchezaji mpambanaji na ameisaidia sana timu, pia niwashukuru GSM kwa kutoa fedha nyingi kuhakikisha anapata matibabu mazuri.