Ambulance yazua kizaazaa, Namungo vs Mbeya Kwanza

Namungo, Mbeya Kwanza yaaihirishwa kisa 'Ambulance'

MCHEZO wa Ligi Kuu Bara kati ya Namungo na Mbeya Kwanza uliokuwa upigwe kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi umeahirishwa baada ya kuchelewa kwa gari la kubebea wagonjwa ‘Ambulance’.

Mchezo huo uliokuwa uanze saa 10:00 jioni ilitokea sintofahamu baada ya wachezaji wa timu zote mbili kuwa uwanjani pamoja na marefa lakini mwamuzi hakupuliza kipenga kuashiria kuanza kutokana na kutokuwepo kwa Ambulance ambayo ipo kwenye kanuni na taratibu za mchezo.

Mawasiliano ya pande zote mbili yalifanyika na saa 10:24 ambulance iliingia Uwanjani hapo lakini mechi haikuendelea na ilipofika saa 10:35 waamuzi waliingia katikati ya Uwanja kisha kutoka na kuelekea vyumba vya kubadilishia nguo.

Baada ya hapo timu ya Mbeya Kwanza ikiongozwa na kocha wake, Mohamed Makata na baadhi ya wachezaji nao waliondoka uwanjani hapo huku wengine wakibaki wakipiga stori na wale wa Namungo.