Aliyewapa raha Simba afunguka

BEKI wa Ihefu, Lenny Kissu aliyewapa raha Simba baada ya kuvunja rekodi ya Yanga iliyojiwekea katika michezo 49 ya Ligi Kuu kucheza bila kufungwa afunguka.

Kissu alivunjwa rekodi hiyo juzi Jumanne katika Uwanja wa Highland Estates, Mbarali dakika ya 62 baada ya bao alilofunga kwa kichwa kutokana na kona iliyopigwa na Never Tiger ambaye naye alikuwa nyota kwenye mchezo huo kwa kufunga bao la kwanza kwa Ihefu kutokana na adhabu ndogo nje ya eneo la hatari.

Kissu alisema wengi waliona ni jambo lisilowezekana hasa kwa kuiangalia Ihefu ikiwa mkiani huku Yanga ikiwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu na ikiwa na rekodi ya kutopoteza michezo kwa muda mrefu.

“Mchezo ulikuwa wa pande zote mbili kwamba kila mmoja angeweza kushinda ila mwenye mbinu za ziada ndio angepata matokeo mazuri, hivyo Ihefu ilikuwa na mbinu mbadala ndio maana tumeweza kushinda.

“Tulitumia udhaifu wa Yanga kwa kupiga mipira mirefu na kulinda muda mwingi ndio maana tuliweza kupata alama tatu sababu tulikuwa tukizihitaji sana na ushindi ambao umeongeza hamasa kubwa kwetu kuelekea michezo inayofuata,” alisema Kissu.

Aliongeza kutofanya vizuri katika michezo iliyopita haikuwa na maana timu yao ni mbovu, bali ni upepo tu uliwakalia vibaya ila kupitia ushindi huu umewasaidia kurudisha matumaini ya kupambana katika michezo iliyobaki.

Alisema baada ya ushindi huo kila mmoja alikuwa na furaha kwa sababu kuifunga Yanga sio kazi ndogo japo soka ni mchezo wa makosa na lolote linaweza kutokea uwanjani na ndicho kilichotokea. Kissu aliaanza kuwika katika soka akiwa Polisi Mara (Biashara United) akiwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambayo hivi sasa ligi hiyo inaitwa Championship.

Alizaliwa Aprili 4, 2000 na hucheza nafasi ya beki, kabla ya kujiunga na Ihefu msimu huu, alikuwa akikipiga Biashara United msimu uliopita. Lenny ni mdogo wa David Kissu kipa wa KMC ambaye aliwahi kuzitumikia timu kadhaa ikiwemo Biashara, Azam, Namungo, Njombe Mji na Toto African.