Zoran: Kwa usajili huu! nataka straika mpya

ACHANA na matokeo ya mchezo wa juzi iliyopata Simba dhidi ya Haras El Hadood, Kocha wa timu hiyo, Zoran Maki amewaangalia nyota wake wapya na kile wanachokionyesha uwanjani na kusema timu itakuwa moto sana, lakini akautaka uongozi umletee straika mmoja matata.

Zoran aliliambia Mwanaspoti kwamba amewaambia mabosi anahitaji mashine nyingine mpya eneo la ushambuliaji ili amalize kazi kabla ya kuanza kwa msimu wa mashindano ikiwamo mechi ya tamasha la Simba Day na ile ya Ngao ya Jamii kuzindua msimu.

Katika mechi juzi usiku, Simba ilicharazwa mabao 2-0 na El Hadood ikiwa ni yao ya tatu ya kirafiki, huku Augustine Okrah na Pape Ousmane Sakho wakiuwasha moto na kumfanya Zoran kushika kichwa kwa furaha na kusema timu imenoga.

Zoran alisema anahitaji mshambuliaji mpya kwa maelezo nyota waliopo wameshindwa kumpa kitu anachotaka tofauti na idara nyingine zilizomfurahisha ikiwamo kiungo. Awali Simba ilimsainisha Cesar Manzoki wa Vipers ya Uganda, lakini ameshindwa kujiunga kambini Ismailia, Misri kutokana na klabu yake kuweka kauzibe na mabosi wa Msimbazi wamekubaliana kumchunia hadi Desemba watakapombeba kama mchezaji huru. “Hadi sasa usajili uliofanyika ni wa kiwango bora. Nimeridhishwa na nyota wapya walioongezwa. Kila mmoja kwa nafasi yake ameonyesha kiwango bora kwa kipindi chote nilichokuwa nao hapa kambini. Timu inaonekana kuwa moto sana,” alisema.

Wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba ni Mzambia Moses Phiri (Zanaco), Nassoro Kapama (Kagera Sugar), Habib Kyombo (Mbeya Kwanza), Victor Akpan (Coastal Union), Nelson Okwa (Rivers United) ambaye ameripoti kambini na ameanza mazoezi jana, Augustine Okrah (Bechem United) na Mohamed Quattara (Al Hilal).

Zoran alisema wachezaji wapya wamekuwa na mwanzo mzuri na kukopi haraka na wengine, hivyo kumpa nafasi nzuri ya kupata kombinesheni ya timu aliyosema imesaliwa na michezo miwili ya kujipima nguvu kabla ya kurejea nchini kwa ajili ya tamasha la Simba Day na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga ili kuzindua msimu wa Ligi Kuu Bara 2022-2023.