Yanga yakwepa mtego wa Simba

Yanga yakwepa mtego wa Simba

Muktasari:

  • Yanga itavaana na Simba kwenye nusu fainali ya kombe la Shirikisho la Azam Mei 28 mwaka huu katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mwanza. YANGA imedhamiria msimu huu kutwaa taji la Ligi Kuu ya NBC walilolikosa kwa miaka minne mfululizo ambapo Kocha wa timu hiyo Nasredine Nabi amesema hatopanga kikosi dhaifu dhidi ya Biashara United kwa hofu ya kupumzisha wachezaji kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba.

Yanga itakuwa ugenini kesho Mei 23 kukipiga na Biashara United katika mchezo wa Ligi utakaochezwa uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza huku Nabi akitamba kuwa hawadharau chochote kwani atapanga kikosi cha maana chenye uwezo wa kumpa pointi tatu ambazo zitawasogeza karibu zaidi na ubingwa.

Akizungumza leo Mei 22 katika kikao na waandishi wa habari jijini hapa kuelekea mchezo huo, Nabi amesema kitu muhimu ambacho wanazingatia kwasasa ni kuhakikisha wanapata pointi tatu na hawatoingia kwenye mtego wa kupumzisha wachezaji ili kuisubiri Simba Jumamosi katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.

Yanga inahitaji Pointi sita tu katika michezo iliyobakia ili kutangazwa mabingwa wapya wa Ligi ya NBC msimu huu huku wakiwa mbele kwa tofauti ya pointi 13 dhidi ya watani wao Simba wenye alama 50 na mechi moja mkononi.

"Tunafahamu mechi tatu zijazo tutacheza kwa uchovu mwingi na tunakabiliwa na kadi za wachezaji hivyo hatuwezi kung'ang'aniza kikosi kilekile, tutabadilisha wachezaji lakini hatuwezi kupanga kikosi dhaifu lazima tubalansi tuanze na timu ambayo itatoa ushindani, mechi nzuri na ushindi" Amesema Nabi na kuongeza;

"Kitu kikubwa ambacho tunazingatia hatuwezi wala kuruhusu kitu kiturubuni eti tunasubiri nusu fainali kwa sasa tunaangalia mchezo wa kesho, hatuwezi kupumzisha wachezaji kwa sababu ya Simba wachezaji wote tunaoona watatupa matokeo kesho tutawatumia,"

Akizungumzia uwanja wa CCM Kirumba amesema kikosi chake hakijapata muda wa kufika kufanya mazoezi kama taratibu zinavyowataka kutokana na uwanja kuwa na matumizi mengine ya mchezo wa leo kati ya Geita Gold na Simba lakini anaamini ni uwanja mzuri ambao hauwezi kuwakwamisha katika jitihada zao za kusaka pointi tatu kesho.

"Tumeshacheza Kirumba mara ya pili Sasa  msimu huu tumesikia uwanja umekarabatiwa lakini hatujapata fursa ya kufika uwanjani kufanya mazoezi, lakini tunachoamini kama uwanja umetengenezwa ni vizuri.

"Lakini kama uko kama tulivyoacha hatuwezi kusema ni mbaya sana, tunaamini huu uwanja haumo kwenye viwanja vibovu ambavyo tumeshatembelea, tunaamini sisi kwetu hautakuwa na shida sana," amesema Nabi.