Yanga yaikodia ndege Rivers

Dar es Salaam. Wadau wa soka nchini wameipongeza Yanga kwa uamuzi wake wa kusafiri na ndege ya kukodi kwenda Nigeria ambako itacheza mechi yake ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United, Jumapili hii

Yanga itaondoka na ndege aina ya Airbus inayomilikiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ACTCL) kesho kwenda Port Harcourt, ambako mechi hiyo itachezwa ikiwa na kibarua cha kuibuka na ushindi wa kuanzia mabao mawili ili iweze kusonga mbele hadi hatua inayofuata

Hilo limethibitishwa na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Yanga, Haji Mfikirwa aliyesema kuwa maandalizi kwa ajili ya safari hiyo yanaendelea vizuri huku akifichua kwamba gharama za jumla za safari ni takribani Sh300 milioni.

“Bado sijapiga hesabu kujua ni kiasi gani, lakini inaweza kufika Sh300 milioni au isifike,” alisema Mfikirwa huku mmoja wa viongozi wa kamati ya utendaji, ambaye aliomba hifadhi ya jina akidokeza kuwa gharama za safari hiyo ukiachana na matumizi mengine zinakaribia Sh300 milioni.

Alisema ndege watakayokodi itaondoka na watu 100, wakiwamo wapenzi na mashabiki wao.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, nyota wa zamani wa soka wamesema kuwa kitendo cha Yanga kwenda kwa ndege ya kukodi kitawasaidia kutowachosha wachezaji wao kama ambavyo ingetokea iwapo wangetumia ndege za kawaida za abiria kwenda Nigeria lakini pia kitawasaidia katika maandalizi yao kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, Septemba 25.

“Wachezaji hawatahisi uchovu kama ambavyo wangetumia ndege nyingine za abiria ambazo huenda zingewalazimu kuunganisha safari na kutumia muda mwingi zaidi, hii ya kukodi itawalazimu kutumia saa nne hadi tano kwenda na muda huo huo kurejea,” alisema kiungo wa zamani wa Yanga, Ally Mayay.

Tathmini iliyofanywa na gazeti hili imebaini kuwa Yanga kama ingetumia usafiri wa ndege za kawaida kama ilivyo kwa abiria wengine, kwanza ingekutana na mtego wa ugumu na umbali wa kufika jijini Port Harcourt, ambako mchezo huo utachezwa kutokana na mazingira ya nchi ya Nigeria yalivyo.

Ikiwa ingetumia usafiri wa ndege za kawaida ambazo ingelazimika kuunganisha ama kwa kwenda Ethiopia au Kenya, Yanga ingelazimika kutumia siku mbili angani kwa kwenda hadi Lagos, Nigeria ambako baada ya kutua hapo ingetakiwa tena kusafiri ama kwa basi au kwa ndege hadi Port Harcourt kutakakochezwa mechi hiyo.

Kutokana na usafiri wa ndege za kutoka Lagos kwenda Port Harcourt kutokuwa wa uhakika, usafiri wa haraka ambao Yanga ingelazimika kuutumia ni wa basi, jambo ambalo ni wazi kwamba lingewachosha wachezaji kutokana na umbali uliopo baina ya mji huo mkuu wa Nigeria na Port Harcourt, ambao upo Kusini Magharibi mwa nchi hiyo.

Umbali kutoka Port Harcourt hadi Lagos ni kilomita 627, sawa na umbali wa kutoka Dar es Salaam hadi Manyoni, Singida, hivyo kwa usafiri wa basi, Yanga ingelazimika kusafiri kwa muda wa saa 11 na dakika saba.

Usafiri binafsi utaifanya Yanga kurudi mapema kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, siku nne baadaye.