Yanga ubabe ubabe tu

Sunday November 22 2020
yanga pic

Cedric Kaze

KUNA dakika 180 ngumu za Ligi Kuu Tanzania Bara leo zikipigwa katika viwanja viwili tofauti lakini kubwa ni saa moja usiku wakati wasiofungika Yanga wakiwakaribisha Namungo wenye hesabu mpya.

Yanga hawajafungika mpaka sasa kwenye ligi na matokeo yao mabaya ni sare. Kikosi hicho cha Kocha Cedric Kaze kitaingia katika mchezo huo kikiwa na akili moja tu kutafuta ushindi wao wa nane utakaowabeba kuwakimbiza Azam ikiwa pia ni maandalizi ya kisaikolojia kabla ya timu hizo mbili kukutana Jumatano ijayo.

Tishio pekee kwa Yanga lilikua ni kupata maumivu kwa kiungo wao Mukoko Tonombe lakini meneja wa timu hiyo Hafidh Saleh amesema mido huyo pamoja na beki na nahodha wao Lamine Moro wako sawa sawa.

Akizungumzia mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Mkapa, alisema hakuna mechi rahisi kwao na mabadiliko ya Namungo katika kuleta kocha mpya Hemed Moroco itaongeza ugumu katika mchezo huo kwa kila mchezaji kutaka kutamba.

Kaze alisema; “Tumesikia wamebadili kocha hii ni changamoto nyingine ya ugumu wa mchezo, hii itafanya kila mchezaji wao kujituma, nafahamu ni timu nzuri (Namungo) wanakaribia kuanza mashindano ya Shirikisho Afrika inamaana mchezo huu ni sehemu ya kujipanga kwao.”

“Tulikuwa na wachezaji wachache waliokuwa na maumivu kidogo na sasa naona kila kitu kipo sawa,tunahitaji kutumia nafasi tunazotengeneza tumeyafanyia kazi hayo tusubiri kuona mrejesho kutoka kwa vijana,” alisema Kaze.

Advertisement

Namungo ambayo imemuondoa kocha wao Mrundi Thienry Hitimana sasa watakuwa na dakika 90 za kwanza chini ya kocha Hemed Morocco kutoka Zanzibar.

Kumpata Morocco tu wakaipeleka timu katika kambi fupi kisiwani Zanzibar kujiandaa na mchezo huo ambao kama watashinda wanaweza kuruka kutoka nafasi ya 9 mpaka ya 5.

Akizungumzia mchezo huo na hata timu alivyoikuta Morocco alisema; “Ukiangalia kikosi sio kibaya kwa mchezaji mmoja mmoja wako sawa kuna vitu vichache sana vya kuvifanyia kazi ili timu irudi katika kasi yake nimekuwa na siku chache hapa siwezi kusema nimefanya kila kitu.”

“Tunakutana na Yanga ni timu nzuri tunaiheshimu lakini nimekuwa nawaona mechi zao walizocheza nawajua muhimu ni vijana wetu wazingatie tulichoelekezana tukiwa katika maandalizi.”

Mchezo mwingine utakuwa pale Uwanja wa Kaitaba ambapo wenyeji Kagera Sugar watawakaribisha Mwadui ukiwa ni mchezo wa kukimbia eneo baya la kushuka daraja.

Timu hizo mbili zinafuatana kule karibu na chini katika msimamo wageni Mwadui wakiwa nafasi ya 15 lakini Kagera Sugar wako chini yao nafasi ya 16 wakitofautiana kwa alama mbili pekee.

Kocha Meck Maxime alisema; “Hatujapata bado kasi ya ushindi ni kama tumekosa bahati hasa tunapokuwa nyumbani lakini hatujakata tamaa tunazidi kushikamana nafahamu hali ya utulivu itakuja na tutashinda sana kwa kuwa bado nina imani na vijana wangu.”

Mwadui wao hawataki kuangalia rekodi hiyo ya Kagera wanachotaka ni kujipanga kuhakikisha wanapata ushindi na kupitia kocha wao Khalid Adam alisema wamejipanga kutaka kuondoka mkiani.

“Mpira wa sasa hakuna aliyenytumbani wala ugenini unaweza kupoteza kokote lakini kwetu sisi tunataka kushinda na ndivyo tulivyojipanga lengo letu ni kutoka eneo ambalo tupo ili kuzidi kupanda juu,” alisema Adam.

..........................................

Na Khatimu Naheka

Advertisement