Upepo wa Yanga waitesa Simba

Upepo wa Yanga waitesa Simba

TAMASHA la wiki ya Mwananchi limeonekana kuendana na upepo mzuri kwa Yanga dhidi ya watani wao wa jadi, Simba tangu lilipoanzishwa 2019.

Ikiwa linafanyika kwa awamu ya nne, Yanga imefanya vizuri katika michezo dhidi ya Simba tofauti na watani wao ambao wameshindwa kufua dafu. Tamasha hilo lilianzishwa 2019 na hadi sasa timu hizo zimekutana mara 11 katika mashindano tofauti ambapo Yanga imeshinda mara nyingi zaidi tofauti na Simba.

Kati ya mara 11, Yanga imeshinda mara tano huku Simba wakishinda mara mbili na mara sare nne.

Katika Ligi Kuu, Yanga wamekuwa watemi zaidi kwa miaka minne ambapo hawapoteza mechi yoyote dhidi ya Simba wakishinda mbili na kutoka sare nne.

Ushindi mwingine wa Yanga ni Kombe la Mapinduzi 2021 waliposhinda kwa penalti 4-3 katika nusu fainali huku pia wakishinda mara moja kwenye Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) mwaka huu, lakini pia Ngao ya Jamii mwaka jana. Ushindi pekee wa Simba dhidi ya Yanga katika miaka minne iliyopita ni katika Kombe la ASFC ambapo mara ya kwanza ilishinda mabao 4-1 katika nusu fainali 2020 na mwaka jana waliposhinda bao 1-0 katika mechi ya fainali ya kombe hilo.