Ukuta wa Yanga wamshtua Chuji

DODOMA. ACHA mvua inyeshe tuone panapovuja. Ndivyo unvyoweza kusema kwani, licha ya Yanga kubeba taji la ASFC mbele ya Coastal Union, lakini kupwaya kwa safu ya ulinzi ya timu hiyo na kuruhusu kufungwa hat-trick, imemshtua nyota wa zamani wa kimataifa, Idd Athuman ‘Chuji’.

Yanga ilifungwa kwa mara ya kwanza mabao matatu katika mechi za mashindano msimu huu wakati ikimaliza dakika 120 za fainali ya ASFC dhidi ya Coastal iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha kabla ya mikwaju ya penalti kuwapa ubingwa wa michuano hiyo.

Mabao yote matatu ya Coastal yaliwekwa kimiani na Abdul Suleiman ‘Sopu’ aliyeweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick kwenye mechi ya fainali ya ASFC na nchini kwa ujumla kwa miaka ya karibuni.

Kitendo hicho kimemfanya Chuji, aliyewahi kung’ara na Polisi Dodoma, Simba na Yanga, kusema ni muda muafaka kwa benchi la ufundi kujitathmini wakati wakijiandaa kwa msimu mpya na hasa michuano ya kimataifa, kwani ikitokea mchezaji msumbufu kama Sopu, itadhalilika.

Chuji aliyewahi kukipiga pia Coastal Union na Singida ambaye kwa sasa ni kocha alisema Yanga imeonesha udhaifu mkubwa katika safu ya ulinzi hivyo kuna kila haja ya mabosi na hasa watu wa benchi la ufundi kufanya usajili katika kipindi hicho kwa ajili ya michuano ya kimataifa.

“Kwa vile itacheza michuano ya Kimataifa wakae chini wafanye skautingi kwenye upungufu ni wapi, kama jana (juzi) safu ya ulinzi ilifanya makosa mengi yaliyoitesa, hivyo iwe kama kengele ya tahadhari ya kuhakikisha inapata beki wa nguvu atakayewabeba CAF,” alisema Chuji na kuongeza;

“Kwa makosa yake ni vigumu kutoboa kimataifa hasa ukikutana na timu yenye washambuliaji wenye kasi na wasumbufu kama alivyofanya Sopu. Nawashauri pia kufanya maandalizi mazuri nikimaanisha kambi ya kueleweka, michezo ya kirafiki ya kueleweka kabla ya mechi za CAF.”

Alipoulizwa ni mchezaji gani aliyekunwa naye msimu huu kwa alichokifanya uwanjani, alisema; “Yule Mayele (Fiston) kadeserve sana kwani alikuwa anatafuta nje ya 18 ndani ya 18 anafunga.”