Tegete: Chunga Sakho, Chama

SIMBA na Yanga zinavaana leo usiku, lakini kocha maarufu nchini, John Tegete amekiangalia kikosi cha Msimbazi na kukiri mabeki wa Yanga wanapaswa kuwa makini na Clatous Chama na Pape Osmane Sakho ambao wamerudi na kasi kubwa msimu huu.

Timu hizo zinavaana kwenye Ngao ya Jamii itakayopigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku Simba ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi kama hiyo kwa msimu uliopita.

Akizungumza na Mwanaspoti, Tegete alisema kwake anaona Chama na Sakho ndio wachezaji wa kuthibitiwa zaidi katika mchezo huo kwani wako vizuri hivyo mabeki wa Yanga wanatakiwa kuwa makini nao kwenye pambano hilo.

“Kwangu nawaona Chama na Sakho ndio wachezaji wa kuchungwa zaidi,nimeona katika mchezo wao na St George walicheza vizuri na wako katika ubora mkubwa hivyo mabeki Yanga wanatakiwa kuwa makini nao wahakikishe hawapati nafasi za kupiga mashuti na kutoa pasi za mwisho,” alisema Tegete baba mzazi wa Jerry Tegete, nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars na kuongeza;

“Kama wakiwadhibiti hao wachezaji wawili nina uhakika mchezo utakuwa rahisi kwa Yanga lakini wakishindwa basi mechi inaweza ikawa ngumu kwao kwani ukiangalia nyota hawa wana kasi na uwezo mkubwa wa kufunga na kutoa za mabao,” alisema Tegete.

Nyota wa zamani wa Kagera Sugar, Ally Mrisho ‘Madonso’ alisema anaona mchezo huo utakuwa mgumu kwa timu hizo mbili kutokana na wababe hao wote wamefanya usajili mzuri na mwenye bahati ndio atakayeshinda pambano hilo.

“Mchezo utakuwa mgumu ukiangalia Yanga wako vizuri na ukiwacheki Simba nao wa moto sasa hapa mwenye bahati ndio ataondoka na ushindi ila pambano litakuwa na mvuto mkubwa sana,” alisema Madonso.