Tambwe: Fiston ni hatari

Muktasari:

  • Amtabiria kuvunja rekodi yake ya mabao

STRAIKA kipenzi cha mashabiki wa Yanga, Amissi Tambwe ametabiri makubwa kwa straika mpya wa timu hiyo, Fiston Abdulrazak.

Tambwe anasema kwa Yanga hii, mabeki wa Ligi Kuu Bara wajipange, kutokana na ujio wa Fiston aliye hatari zaidi akitokea pembeni upande wa kushoto, hivyo akicheza na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ safu hiyo itakuwa ngumu kuzuilika.

Yanga imemsajili Fiston akitokea ENPPI ya Misri, huku Saido akitokea Vital ‘O’ ya Burundi, wawili hao wametazamwa kuleta mabadiliko katika safu ya mbele ya timu hiyo chini ya Kocha Mrundi, Cedrick Kaze.

Tambwe anaamini kama Fiston akiendeleza makali yake Yanga anaweza kuikuta moja ya rekodi zake kwenye kutupia.

Tambwe ambaye kwa sasa anacheza Polisi ya Djibouti alisema Saido ndiye aliyebeba ramani ya ubingwa wa klabu hiyo na ujio wa Fiston ni kumsaidia majukumu ya kupeleka mipira mbele na pasi zake za kutokea upande wa kushoto.

Tambwe alimwelezea Fiston anaweza akacheza kama namba tisa na akafunga, lakini sio mtaalamu sana kama anavyofanya akitokea pembeni upande wa kushoto, ambako Saido itakuwa rahisi kupokea mipira ya kufunga. “Ramani ya ubingwa ipo mikononi mwa Saido, kutokana na uzoefu alionao, akili, mbinu pia ana uwezo mkubwa wa kuituliza timu ikiwa kwenye presha kubwa ya kupata matokeo, sasa faida ya Fiston ni uwepesi wake wa kupiga pasi na kusumbua ngome za ulinzi,” alisema na aliongeza,

“Nilibahatika kuzitazama mechi za Yanga baadhi, ndio maana nasema kusajiliwa kwa Fiston kunakwenda kukamilisha safu yao ya ushambuliaji kuzalisha mabao mengi,” alisema. Jambo lingine aliloliona Tambwe Yanga ni inahitaji mshambuliaji namba tisa, la sivyo Kocha Cedrick Kaze aanze kumjenga Michael Sarpong aliyemuelezea bado hajaonyesha ubora ule ambao Yanga waliutarajia.

“Sarpong anacheza lakini hayupo kwenye ubora unaotakiwa kwenye kikosi cha Yanga ambacho nakiona nikizuri kuanzia kwa mabeki, viungo na sasa ushambulaiji unakamilika,” alisema.

Kuhusu upande wa Kocha Kaze, Tambwe alisema ni kocha anayetambulika kwa nidhamu ya kazi, kujituma kujenga umoja na thamani ya wachezaji kujisikia ni sehemu ya timu.

“Yanga msimu huu haina sababu ya kukosa ubingwa kwa sharti la kuwa watulivu, kwa sababu kocha ni mzuri wa kufanya wachezaji wawe na mpira mzuri mguuni ikiwemo kuwafanya wajiamini kila mechi,” alisema Tambwe ambaye aliweka rekodi ya kufunga hat-trick nyingi wakati akzichezea Simba na Yanga kwani hadi anaondoka alikuwa amepiga hat-trick saba.

Alipoulizwa je Saido na Fiston wanaweza kuvunja rekodi yake ya mabao na hat-trick kwenye Ligi Kuu Bara, Tambwe alijibu

“Ni vitu ambavyo vinafanyika na binadamu hivyo bidii ya mtu ndio inafanya afikie rekodi ya mtu mwingine. Hivyo kazi kwao.”

Tambwe aliwahi kuibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo katika timu mbili tofauti.Alianza kuwa mfungaji bora akiwa Simba baada ya kumaliza ligi na mabao 19 msimu wa 2013/2014, pia msimu uliofuta aliibuka mfungaji bora akiichezea Yanga baada ya kupachika wavuni mabao 21 huku akifunga hattrick saba katika timu zote hizo mbili kipindia nacheza hapa nchini.