Takukuru kuishukia TFF juu ya taarifa za fedha za Caf

TFF yaweka sawa ishu ya Karia

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Brigedia Jenerali John Mbungo amesema wameanza uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mbungo alisema timu ya uchunguzi ya Takukuru itawahoji viongozi wa TFF ili kutafuta ukweli wa madai, ambayo TFF imekuwa likihusishwa nayo, ikiwa ni siku chache tangu Shirikisho la soka la Kimataifa (Fifa) kumfungia miaka mitano, rais wa Afrika (Caf), Ahmad Ahmad.

Fifa imemfungia Ahmad ikimtuhumu kwa rushwa, kutoa zawadi na upendeleo, ubadhilifu wa fedha na kutumia vibaya nafasi yake kama rais wa Shirikisho la soka Afrika (Caf).

Baada ya hukumu hiyo, TFF ililazimika kutoa ufafanuzi wa taarifa iliyosambaa mitandaoni juzi wakihusishwa na mgao wa malipo yaliyosababisha Ahmad kufungiwa.

Taarifa iliyotolewa na TFF na kuthibitishwa na ofisa habari wao, Clifford Ndimbo ilikiri shirikisho hilo kupokea dola 100,000 kutoka Caf kwa maendeleo ya michezo.

“Mei 2017 CAF ilipitisha uamuzi wa kila mwanachama wake kupatiwa fedha hiyo, Dola 80,000 ilipelekwa kwenye maendeleo ya soka na Dola 20,000 ilienda kwa rais wa shirikisho la nchi husika ili kumsaidia kwenye majukumu yake kwa kuwa halipwi mshahara.

“Rais Karia alielekeza Dola 20,000 zitumike kwenye shughuli mbalimbali za Shirikisho, hakuna fedha iliyowahi kuingizwa kwenye akaunti binafsi ya rais, kama inavyovumishwa,” ilieleza taarifa ya TFF juzi.

Jana, Mkurugenzi wa Takukuru, Bgrigedia Jenerali Mbungo aliliambia Mwananchi kwamba licha ya TFF kutoa maelezo kukanusha taarifa hizo, taasisi hiyo imeyapima maelezo yao ili kujiridhisha na kubaini ukweli wa kilichoongelewa na TFF. “Sisi (Takukuru) ni tofauti na watu wengine ambao habari ikitokea mtandaoni wataipuuza, sisi hatupuuzi jambo lolote linalozungumzia ubadhilifu wa fedha za umma au taasisi yoyote, tunaifuatilia.

“Timu yetu ya uchunguzi itawahoji TFF ili kujiridhisha kwenye hiki kinachoendelea kuhusu sakata la rais wa Caf, lakini pia tutaendelea kulichunguza kupitia vyanzo vingine ili kujua ukweli huo,” alisema.

Brigedia Jenerali Mbungo alisema taasisi yao ni ya uchunguzi, hivyo hawadharau chanzo chochote cha taarifa hata kama ni mtandao, watakichunguza na kutafuta ukweli.

“Pamoja na kwamba taarifa hizo zimetokea Caf, lakini tumeona sehemu zinaongelea nchi yetu, hivyo hatuwezi kuidharau, timu ya uchunguzi imefuatilia na inaendelea na uchunguzi wake na wakati wowote itawahoji TFF katika hili,” aliongeza.

Ingawa juzi rais wa TFF, Wallace Karia aliliambia gazeti hili kwamba katika hukumu ya Fifa kwa rais wa Caf, hakuna sehemu ambayo imeitaja TFF, Tanzania wala Taifa Stars. “Sijui hizi habari zinatoka wapi, lakini kuna watu wanataka kunitia doa ila naamini watashindwa kwa kuwa najiamini na kila ninachokifanya namtanguliza Mwenyezi Mungu,” alisema Karia.

Alisema anafahamu yuko katika mapambano ambayo anaamini yatapita na kitakachofuata baada ya mapambano ni kuipeleka Tanzania kwenye Kombe la Dunia na si vinginevyo.

Wakati Karia akisema hayo, jana mchana ilisambaa barua iliyodaiwa kuwa ilitoka TFF kwenda Caf kwa ajili ya kuelekeza mchanganuo wa Dola 100,000 walizoomba kuingia katika akaunti mbili tofauti.

Barua hiyo, ambayo ilionekana kusainiwa na katibu wa TFF, Wilfred Kidao, ilionyesha kuwa fedha hizo zilitakiwa kuingia kwa makundi. Dola 80,000 kuingia katika akaunti ya shirikisho na 20 katika akaunti ya rais.

Hata hivyo, katibu huyo wa TFF, Kidao hakupatikana kwa simu kwa ajili ya kuitolea ufafanuzi barua hiyo licha ya simu yake kuita lakini haikupokelewa.

_____________________________________________________________

Na Imani Makongoro