Simba: Yanga! Viongozi waweka kikao kizito Dar

Simba: Yanga! Viongozi waweka kikao kizito Dar

SIMBA imeweka msimamo wa kutoomba mchezo wao dhidi ya Yanga Aprili 30 usogezwe mbele, ikitamba siku sita tu zinawatosha kujiandaa na kuichakaza Yanga kwenye mchezo huo wa duru ya pili ya Ligi Kuu Bara utakaopigwa Kwa Mkapa.

Simba itavaana na Yanga baada ya kumaliza mechi yao ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini ikiwa ni siku sita tu kabla ya derby hiyo kupigwa na kulikuwa na tetesi walikuwa wakiomba mechi iahirishwe.

Kama Simba itashinda, itapunguza gepu la pointi kwa Yanga na ikifungwa, itaongeza ugumu wa kuifikia na kuiondoa Yanga kileleni katika harakati za ubingwa, lakini mabosi wa Simba wamesisitiza mechi uitapigwa kama ilivyopangwa.

Yanga yenyewe imeshaanza programu ya mechi hiyo, lakini Simba itakuwa na mechi tatu, zikiwamo mbili za kimataifa dhidi ya Orlando na nyingine ya robo fainali ya Kombe la ASFC dhidi ya Pamba iliyoahirishwa kupigwa jana usiku.

Mabosi wa Simba wamekiri ratiba kwa upande wao ni ngumu, lakini wanaimudu na wataiduwaza Yanga.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mulamu Nghambi alisema; “Siku sita zinatutosha sana kuifanyia Yanga maandalizi na tukaifunga, wala sio tatizo kwetu, japo ni kweli kwa upande wa nje timu itakuwa na ratiba ya mechi ngumu, lakini sio tatizo kwa klabu yetu.”

Alisema wanaanza na Orlando, watakapoitoa na kutinga nusu fainali ya CAF, kibao kinageukia Yanga, hivyo wasijidanganye, eti siku sita kwa Simba zitawasumbua, kauli iliyoungana na ile iliyotolewa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu aliyesisitiza watacheza mechi na Yanga kwa mujibu wa ratiba.

“Tutafuata ratiba inavyotaka, maana imepangwa iwe hivyo,” alisema Mangungu na kusisitiza kwamba kwa sasa wameelekeza nguvu kwenye robo fainali ya CAF.


MSIKIE BATGOL

Nyota wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ amekiri matumaini ya Simba kutetea ubingwa wake msimu huu ni magumu na wanapaswa kumwaga jasho jingi kutimiza hilo huku akiwapa ujanja wa kumsimamisha mtani wao, Yanga.

Batigol alisema sare dhidi ya Polisi iliwaumiza Simba na kudidimiza matumaini yao kwenye mbio za ubingwa lakini bado wana njia nyingine ya kufanya hivyo ambayo ni kumfunga Yanga kwenye mchezo wa Aprili 30 vinginevyo wasahau kabisa.

Nyota huyo ambaye ni kocha msaidizi wa Lipuli kwa Sasa, alisema; “Kiukweli kwa mbio za ubingwa asilimia kubwa inaonekana ziko kwa Yanga lakini bado Simba wasikate tamaa wanatakiwa wapambane ili mechi yao ya dabi wahakikishe wanapata pointi tatu ili kuendelea angalau kupambania ubingwa.”


ISHU YA VAR

Mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania, Omary Abdulkadir ameionya Simba kuwa makini na teknolijia mpya ya VAR itakapoikabili Orlando wikiendi hii, huku mabosi wa klabu hiyo ya Msimbazi, jana mchana walikuwa na kikao kizito jijini Dar es Salaam kuweka mipango sawa kabla ya kuwaa Wasauzi.

Katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho, CAF (Shirikisho la Soka Afrika) limetangaza kutumia teknolojia ya video kkwa usaidizi wa waamuzi VAR ikiwa ni mara ya kwanza itatumika nchini.

Uwepo wa VAR, umemuibua Abdulkadir, aliyeitahadharisha Simba akisema inapaswa kucheza kwa tahadhari zaidi hasa kwenye eneo la ndani au jirani na lile la penalti boksi akisisitiza kwamba mechi nyingi mabeki wa timu hiyo wamekuwa wakicheza faulo kwenye mita 30, 25 hadi 20.

“Bahati mbaya wamekuwa pia wakifungwa mabao ya frii kiki, jambo ambalo kwenye mechi na Orlando hawatakiwi kulifanya hasa ukizingatia VAR itakuwa inaonyesha kila tukio, hivyo wacheze kwa tahadhari kubwa,” alisema mwamuzi huyo mstaafu, aliyeungwa mkono na mwamuzi mwingine, Ibrahim Kidiwa.

“Uwanjani kuna mambo mengi, lakini wachezaji wetu tena kuna wangine uwa wanacheza faulo za ajabu wakiamini hawataonwa na refarii, kwenye teknolojia ya VAR, Simba wawe makini sana,” alisema Kidiwa na kuongeza; “Kuna matukio mchezaji anaona mpira huko upande mwingine anampiga ngumi mchezaji wa timu pinzani na mambo kama hayo, kwenye soka letu yapo sana, hivyo wachezaji wa Simba wajipange ipasavyo, VAR ipo kwa ajili ya matukio kama hayo.”

Nini maoni yako kuhusiana na mchezo huu wa Simba na Pirates Jijini Dar es Salaam. Tutumie kwenda; 0658-376 417