Simba, Wanigeria ni buku saba tu

Simba, Wanigeria ni buku saba tu

MABOSI wa Simba wamewaita mashabiki wa klabu hiyo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambako watarudiana na Plateau United katika Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwaambia kwa buku saba tu wanaliona goma, huku wakisisitiza wanataka kumaliza dakika 90 zilizosalia kibabe nyumbani.

Simba na Plateau inayotarajiwa kuwasili leo kutoka kwao Nigeria, zitavaana kesho Jumamosi katika mechi ya marudiano huku wenyeji wakiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 iliyopata ugenini wikiendi iliyopita kwa bao la Clatous Chama.

Mechi hiyo imepangwa kuanza kupigwa saa 11:00 jioni na Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda alisema licha ya kupata ushindi ugenini, hawatabweteka kwenye mchezo huo wa marudiano kwa vile wanataka kumaliza mchezo kibabe.

“Tunatakiwa tupambane ndani ya dakika 180, sio 90, hawa wapinzani wetu wapo vizuri na hatutakiwi kuwabeza hata kidogo kiukweli,” alisema Kaduguda maarufu kama Simba wa Yuda.

Kaduguda alisema kwa timu iliyotwaa ubingwa wa Nigeria mara tatu mfululizo mbele ya Enyimba sio ya kubezwa na kwamba makocha wao wataiandaa timu kupata ushindi nyumbani na kuwaalika mashabiki wajitokeze kwa wingi kuwaongeza nguvu nyota wao.

MSIKIE MANARA

Naye Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara aliwataka mashabiki wa Simba kujitoteza kwa wingi siku ya mchezo akitaja uwanja mzima uwe na rangi nyekundu na nyeupe, huku akitaka viingilio kuwa ni Sh 7000, kwa kiingilio cha chini kabisa.

BY THOMAS NG’ITU NA RAMADHAN ELIAS