Simba: Tuongeze sauti?

Muktasari:

  • Kocha Mkuu kwasasa ndiye anayesubiriwa aje kuliamsha

SHIRIKISHO la Soka la Afrika (Caf) limewapa kiburi Simba kutamba dhidi ya klabu zote za Ukanda wa Afrika Mashariki. Caf imewaruhusu Simba baada ya kuingia kwenye hatua ya makundi kuongeza mastaa 10 wa kigeni kama wanataka.

Hao watacheza Klabu Bingwa Afrika tu na usajili wao unamalizika Jumapili ya Januari 31. Usajili huo unaipa kiburi Simba cha kuwa na miziki miwili mizito ndani ya Uwanja mmoja ukicheza kimataifa na mwingine ligi ya ndani. Ndio maana kwenye mitandao ya kijamii viongozi wa Simba walikuwa wakitambia Yanga kwamba tuongeze sauti au inatosha? Wakimaanisha wanasikia kishindo cha usajili wa Afrika wanaoendelea kuufanya?

Simba wanatambia usajili wa nyota watano wapya katika kipindi hiki cha dirisha dogo kilichofungwa Januari 15,unaweza kuwapa vikosi viwili vya kibabe vitakavyowafanya washiriki Ligi ya Mabingwa Afrka, Ligi Kuu Bara na mashindano mengine bila presha wala hofu.

Kwa kuwanasa nyota hao, Simba imetimiza orodha ya wachezaji 30 ambao itawatumia katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini bado kuna wawili wanaweza kuongezekana dakika yoyote kabla ule wa kimataifa haujafungwa.

Ndani kwenye Ligi na Kombe la Shirikisho itawatumia wachezaji 27 tu kutokana na kubanwa na matakwa ya kikanuni.

Watano wapya ni beki Peter Muduwa kutoka Zimbabwe, viungo Doxa Gikanji (DR Congo) na Lwanga Thaddeo kutoka Uganda na washambuliaji Lokosa Junior (Nigeria) na Perfect Chikwende (Zimbabwe).

Kwa vile Chikwende hatoichezea Simba katika Ligi ya Mabingwa kutokana na kuwa ameshaitumikia FC Platinum kwenye mashindano hayo, jina lake litaingizwa katika usajili wa mashindano ya ndani na atachukua nafasi ya Francis Kahata ambaye yeye ni kimataifa tu.

Mchezaji mwingine kati ya wapya waliosajiliwa ambaye jina lake litaingizwa katika usajili wa ndani wa Simba ni Lwanga ambaye anachukua nafasi iliyoachwa na kiungo Mbrazil, Gerson Fraga anayeuguza majeraha baada ya kufanyiwa operesheni ya goti.

Kwa vile Lwanga hajachezea timu yoyote Caf yeye amebahatika kucheza mashindano ya ndani lakini pia anafuzu moja kwa moja kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Waliobakia ambao ni Muduwa, Lokosa na Gikanji wenyewe watachezea Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika tu kwani hawafuzu vigezo vya kucheza mashindano ya ndani na Mnyama bado amepania kuongeza wengine kutoka DR Congo ambao watakuwa na mikataba mifupi.

Kikosi cha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambacho mashabiki wa Simba na wadau wa soka wanatamani kuona kitakuwaje, kinaweza kuundwa na kipa Aishi Manula na mabeki Shomary Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango na Peter Muduwa ambao juu yao kutakuwa na viungo Jonas Mkude, Doxa Gikanji, Clatous Chama, Luis Miquissone na Hassan Dilunga wakati mbele anaweza kusimama Lokosa au John Bocco.

Lakini wakati hali ikiwa inaweza kuwa hivyo upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, katika mashindano ya ndani kikosi cha Simba kinaweza kuundwa na Beno Kakolanya, Ibrahim Ame, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Pacsla Wawa, Lwanga Taddeo, Perfect Chikwende, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere au Chris Mugalu, Miraji Athuman na Hassan Dilunga

Vikosi hivyo viwili vinaweza kusaidiwa na wachezaji kadhaa watakaoingia kutokea benchi ambao ni Ally Salim, David Kameta, Kennedy Juma, Ibrahim Ajibu, Bernard Morrison na Francis Kahata.