Simba, Polisi ni suala la muda tu

Muktasari:

  • Kikosi cha Polisi Tanzania kinachonolewa na kocha wa muda, John Tamba kitaikaribisha Simba katika mchezo wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi kuanzia saa 10:00 jioni, leo.

Dar es Salaam. Kikosi cha Polisi Tanzania kinachonolewa na kocha wa muda, John Tamba kitaikaribisha Simba katika mchezo wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi kuanzia saa 10:00 jioni, leo.

Simba inashuka katika mchezo huo huku rekodi zikiibeba ikiwa imeshinda mechi tano na sare moja katika mechi sita ilizokutana na Polisi Tanzania.

Polisi Tanzania ilipanda Ligi Kuu 2020/2021, lakini tangu hapo haijawahi kuifunga Simba katika mchezo wowote.

Katika mchezo wa Polisi dhidi ya Simba uliopigwa Februari 4, 2020 Simba ilishinda mabao 2-1 ikiwa nyumbani, Julai 26, 2020 Simba ilishinda mabao 2-1 ugenini, ilhali Desemba 9, 2020 Simba ilishinda 2-0 ikiwa nyumbani, Juni 19, 2021 Polisi ilifungwa bao 1-0 ikiwa nyumbani, Oktoba 27, 2021 Simba ilishinda 1-0 nyumbani na Apili 10, 2021 zilitoka suluhu Simba ikiwa ugenini.

Akizungumzia mchezo huo nyota wa Polisi Tanzania, Tariq Simba alisema wamejiandaa vizuri na lengo ni kufanya vizuri.

“Simba ni timu kubwa na siku zote tunapokutana huwa wanakuwa na ushindani wa kutosha. Tumekuwa na rekodi mbaya kwao, lakini historia sio kitu maana hata kwenye Kombe la Dunia tunaona timu zikivunja rekodi ambazo zimewekwa,” alisema Simba.

Kocha mkuu wa Simba, Juma Mgunda alisema mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa, lakini lengo lao ni kuhakikisha wanashinda licha ya kuwa na ushindani mkubwa.

“Tunatambua tutakuwa na ushindani. Tunawaheshimu Polisi ni moja ya timu zenye ushindani, lakini tumejiandaa na vijana wanajua kabisa tunacheza mechi ya aina gani. Niwahakikishie tupo tayari kushindana na Polisi,” alisema Mgunda.

“Hii ni ligi na ina ushindani. Kwa hiyo kutoka sare nyumbani au ugenini ni sehemu ya mpira. Tunataka matokeo kwenye mchezo huu na tunajua tunacheza na watu waliojiandaa.” Mgunda alisema anaiheshimu Polisi na haangalii matokeo iliyopata katika mechi ilizocheza. Katika msimamo wa ligi Polisi inashika nafasi ya 14 ikiwa na pointi tisa ilhali Simba ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 28 kwenye mechi 13 ilizocheza.