Sikieni anachokisema Mpole

MFUNGAJI Bora wa Ligi Kuu Bara, George Mpole anayekipiga Geita Gold amewataka wachezaji wenzake wa timu ndogo kuamini wanaweza na kuondoa kasumba kuwa ili wang’are lazima wawe kwenye timu vigogo za Simba, Yanga na Azam FC.

Mpole alisema kasumba hiyo ya kuamini vigogo tu ndio wanaoweza, ndizo zinazofanya hata mashabiki kuweka turufu ya ubingwa kwa timu hizo, lakini kumbe hata timu za chini zikiamua kupambana zinaweza kufanya kweli.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mpole alisema wadau wa soka wanatakiwa kubadilika na kuondoa mawazo ya hizo timu tatu pekee kwani kila timu ambayo inashiriki ligi hiyo inakuwa na uwezo na ndio maana imefikia hatua hiyo.

Alisema yeye akilini mwake anaamini mchezaji anaweza kupata mafanikio kupitia timu hizo ndogo bila hata ya kucheza hizo timu kubwa.

“Simba, Yanga na Azam ni timu kubwa sana katika ligi yetu, lakini zisitufanye wachezaji wa timu ndogo tukakata tamaa na kujiona kama hatuwezi, kila Mtanzania ajue kila timu ligi kuu inaweza kutoa mfungaji bora au timu nyingine inaweza imani ya kuamini Simba na Yanga sio kweli kabisa,” alisema Mpole.

Alisema hata kuibuka kwake Mfungaji Bora imeshtua kwa aina ya timu anayoitumikia, lakini ni neema za Mungu na uwezo wake binafsi ambao umemfikisha hapo alipofika hivi sasa, hivyo anatambua deni kubwa alilonalo kwa Watanzania.

“Msimu unaokuja popote nitakapokuwa najua nina kitu ambacho Tanzania inanitegemea nacho, kwa uwezo wa Mungu naamini nitafika ninakokusudia kufika, wazawa tunaweza,” alisema Mpole aliyefunga mabao 17 Ligi Kuu.