Pan waigomea Ken Gold wakitoshana nguvu

Sunday January 16 2022
Pan PIC
By Saddam Sadick

Mbeya. Licha ya kutangulia kupata bao la mapema dakika ya tano, lakini Ken Gold imekubali kutoshana nguvu dhidi ya Pan Africa baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Katika mchezo huo uliopigwa leo Jumapili katika uwanja wa Sokoine jijini hapa, ulikuwa wa mwisho kuhitimisha raundi ya kwanza ya Championship.

Timu hiyo ya wilayani Chunya mkoani hapa, ilipata bao dakika ya tano kupitia kwa Straika wake, Mishamo Michael lililodumu hadi mapumziko.

Hata hivyo dakika ya 13, staa na mkongwe wa timu hiyo, Dany Mrwanda aliikosesha bao la pili kufuatia shuti lake mkwaju wa penalti kupanguliwa na Kipa wa Pan Africa, Alex Venance.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Pan Africa wakionekana kushambulia kuwazidi wenyeji japokuwa umakini ulikuwa mdogo katika kutumia vyema nafasi za mwisho kupata mabao.

Ilikuwa dakika ya 86, ambapo Mshambuliaji wa timu hiyo, Munir Fikirini alipoisawazishia bao akiunganisha kwa kichwa krosi fupi ya Ayoub Mohamed.

Advertisement

Ken Gold walijaribu kulazimisha mashambulizi kwa kutengeneza nafasi kadhaa lakini uimara wa Kipa Venance na mabeki ambao walikuwa makini kuokoa hatari zote.

Kwa matokeo hayo, Ken Gold wanafikisha pointi 17 wakichumpa nafasi moja hadi nafasi ya saba, huku Pan Africa wakifikisha alama 14 baada ya timu zote kucheza mechi 15.

Advertisement