Pablo: Chama? Namuanzisha!

Sunday January 16 2022
Chama1 pic
By Clezencia Tryphone

KOCHA Pablo Franco wala hataki kuremba, kwani amemjumuisha Clatous Chama kwenye kikosi kilichoenda Mbeya na huenda akamtumia nyota huyo aliyerejea Msimbazi kutoka RS Berkane ya Morocco iliyomsajili mwishoni mwa msimu uliopita.

Simba inatarajiwa kuvaana na Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara kesho Jumatatu kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na Kocha Pablo aliliambia Mwanaspoti kuwa Chama ni mchezaji mzuri na inawezekana akampanga katika kikosi mchezo ujao endapo atajiridhisha na utimamu wake wa mwili kimchezo.

Pablo alisema hana shaka na uwezo wa Chama, lakini atataka kutumia mazoezi siku mbili kuanzia jana jioni na leo ndipo atajua kama atampanga au la.

“Ni ngumu tu mchezaji anafika hata hujamuangalia mazoezini useme moja kwa moja utampa nafasi hapana, nikimuona yupo fiti nampanga,” alisema Pablo.

Kocha huyo alikiri Mbeya City ni kati ya timu ngumu za mikoani zinazofanya vizuri msimu huu na amekuwa akiifuatilia na anaamini dakika 90 zitaamua kati yao.

Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 24 nyuma ya Yanga yenye pointi 29, ilihali Mbeya City ipo nafasi ya tano ikikusanya alama 16 ikipoteza mechi moja na kutoka sare saba na kushinda michezo mitatu.

Advertisement
Advertisement