Nugaz afichua ishu ile ya Saido

OFISA Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz ambaye ni mmoja watu wa karibu wa Saido Ntibazonkiza amefichua kuwa alichokifanya mchezaji huyo kwenye mechi ya juzi ni kuonyesha hisia zake.

Alisema kwamba alionyesha ishara za kwamba hapendi kabisa kuanzia benchi haswa akiwa fiti kwenye kuasisti na kufunga.

“Ametoa ujumbe kwamba muda mwingine unapomuweka benchi hafurahishwi, lakini wachezaji wanaocheza ndani ni 11 na ndio maana yeye kaingia na kaonyesha kitu bora,” alisema Nugaz.

Saido alifunga bao la tatu katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Gwambina na badala ya kushangilia bao lake hilo alionyesha ishara ya kutaka atolewe, pia akionyesha kidole kichwani kinachotafsiriwa kuwa yeye ana akili ya mpira.

Wakati akifanya kituko hicho, wachezaji wenzake walimvamia ili kushangilia bao hilo na akanyanyuliwa na mshambuliaji mwenzake, Michael Sarpong.

Alipoteremshwa chini alitoka nje ya uwanja lakini kipa Faruk Shikhalo alimtaka arejee, Saido bado alifosi kutoka nje na ndipo beki Kibwana Shomari alimfuata na kumtaka arejee uwanjani lakini bado mchezaji huyo alionekana kurejea huku akiwa hana furaha.

Wakati Saido akiomba kutoka, idadi ya wachezaji wa kufanyiwa mabadiliko walikuwa wameshamalizika baada ya kuingia Bakari Mwamnyeto, Sarpong na yeye mwenyewe aliyekuwa ameingia sub pia.

Baada ya mchezo kumalizika benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Juma Mwambusi walimfuata na kuzungumza naye kwa takribani dakika moja kisha mchezaji huyo alitoka uwanjani na kuvua shati lakini mashabiki walimsindikiza kwa kumpigia makofi.

Lakini Mwambusi alisema kitendo cha mchezaji huyo ilikuwa ni furaha iliyopitiliza ingawa na Saido naye akazuga kwamba ya uwanjani yaliishia kulekule.

Kitendo alichokifanya Saido ni kama kinamchonganisha kwa kocha mpya wa timu hiyo, Nasreddine Nabi ambaye kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema kwake yeye nidhamu ndio kitu kikubwa.


JOB, KISINDA

MASTAA wa Yanga, Dickson Job na winga Tuisila Kisinda walioumia dhidi ya Gwambina wako freshi. Dickson Job aliumia nyama za paja dakika ya 41 ya mchezo huku Tuisila Kisinda akiumia bega dakika ya 65 ambapo wote hawakuweza kuendelea na mchezo huo kutokana na maumivu waliyoyapata.

Mwanaspoti lilitaka kujua wanaendeleaje ambapo taarifa za awali kutoka kwa daktari wa timu hiyo Shecky Mngazija, licha ya kukataa kuzungumzia zaidi suala hili kutokana na kanuni na taratibu za klabu hiyo lakini amesema wanaendelea vizuri na wanaweza kutumika katika mechi zijazo.