Ngorongoro hawapoi

Ngorongoro hawapoi

Muktasari:

Timu nne za kwanza za Afcon zitafanikiwa kufuzu moja kwa moja kwa fainali za Kombe la Dunia za U-20 zitakazofanyika nchini Indonesia

Dar es Salaam. Baada ya kufuzu katika fainali ya mashindano ya Afrika (Afcon), kocha mkuu wa timu ya taifa ya U-20 (Ngorongoro Heroes), Jamhuri ‘Julio’ Kihwelu amesema sasa wanaelekeza nguvu zao kutafuta tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia.

 Julio amefanikiwa kuiongoza Ngorongoro Heroes kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika ambazo zitafanyika nchini Mauritania kuanzia Februari 14 hadi Machi 3 na timu nne zitafuzu moja kwa moja kwa Kombe la Dunia nchini Indonesia zilizopangwa kuanza Mei 20 hadi Juni 12 mwakani.

Kocha huyo alisema pamoja na kufungwa mabao 4-1 na Uganda katika mechi ya fainali, bado anawaamini vijana wake kuwa na uwezo mkubwa na watafanya maandalizi ya kina ili kufanya vizuri nchini Mauritania.

Alifafanua kuwa Watanzania wanatakiwa kuwa na imani na timu yao kwani kufungwa katika mechi ya fainali kulitokana na ugumu wa mechi ya nusu fainali dhidi ya Sudani Kusini na wachezaji kadhaa walipata majeraha.

“Baadhi ya wachezaji walipata na majereha katika mchezo mgumu wa nusu fainali na kushindwa kucheza vyema katika mechi ya fainali, hata hivyo dhamira yetu ilikuwa kufuzu fainali ya Afcon, na sasa tumefanikiwa.

“Miaka ya nyuma nilisema kuwa moja ya malengo yangu katika kufundisha mpira ni kuiwezesha Tanzania kufuzu kombe la Mataifa ya Afrika na kombe la dunia, nashukuru nimefanikiwa kufuzu Afcon na sasa naelekeza nguvu kombe la Dunia,” alisema Kihwelu.

Rais wa TFF, Wallace Karia alisema kuwa wameweka mikakati ya kuhakikisha timu hiyo inafanya vyema fainali za Afcon ambapo timu ambazo zitafuzu hatua ya nusu fainali, zitafuzu moja kwa moja fainali za Kombe la Dunia.

Karia mbali ya kuwapongeza wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo, alisema kuwa moja ya mikakati yao ni kuiwezesha timu hiyo kuweka kambi nje ya nchi na kushiriki mashindano maalum ya U-20 Falme za Kiarabu.

Alisema kuwa kambi ya timu hiyo imepangwa kuanza hivi karibuni ambapo watarejea katikati ya Januari mwakani tayari kwa mashindano ya Uarabuni. Hata hivyo hakuweza kuitaja nchi ambayo Ngorongoro Heroes itaweka kambi.

“Najua wadau wa soka watataka kujua kwa nini kombe limekwenda Uganda na wala si Tanzania. Kwa kifupi wachezaji walicheza kwa kujituma sana na kupigania taifa lao kwa lengo la kufuzu na kutwaa kombe, hata hivyo mechi ya fainali ilikuwa ngumu sana na wachezaji wetu wengi walikuwa majeruhi.

Kufungwa ni sehemu ya mchezo, lakini dhamira ilikuwa kufuzu Afcon pamoja na malengo ya kutwaa ubingwa kuwepo. Kombe tuliwahi kushinda mwaka jana nchini Uganda na kukaa nalo mwaka mzim. Nawaomba wadau tuanze kufikiria fainali za Afrika na kufuzu kombe la dunia,” alisema Karia.

By Majuto Omary