Nabi aja jambo zito Yanga

Friday November 26 2021
Nabi YNGA PIC
By Khatimu Naheka

KOCHA wa Yanga, Nesreddine Nabi ana jambo lake. Hesabu zake ziko mbali, kuanzia jana anakomaa na viungo wake na mastraika akisuka mipango ya kukabiliana na Uwanja wa Sokoine wanakokwenda kukipiga na Mbeya Kwanza, Jumanne ijayo. Nabi ameshtukia kitu akiona kwamba katika mchezo uliopita mbali na suala la uwanja mbovu wa Ilulu wakati wakidondosha pointi mbili lakini viungo wake hawakutengeneza nafasi nyingi.

Akizungumza na Mwanaspoti Nabi alisema ratiba yao ya jana ya mazoezi wamekuwa wakitafuta mbinu nyingi za kutengeneza mabao akianzia na eneo la kiungo na kuwaongezea mbinu za ushindi ili kuendeleza kasi yao.

Mbali na viungo pia Nabi alisema washambuliaji wake wamekuwa na mazoezi magumu ya kumalizia nafasi kitu ambacho nacho alikigundua katika mchezo uliopita dhidi ya Namungo ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

“Uwanja ulitupa shida ni lazima tujiandae pia kwa mazingira ya kukutana na viwanja vya namna hiyo,sawa uwanja ulitupa wakati mgumu lakini hata sisi yapo mambo ambayo hatukufanya kwa ubora,”alisema Nabi ambaye anajua Kifaransa, Kiarabu na Kingereza.

“Tumekuwa na mazoezi ya kuangalia upya akili yetu ya kutafuta nafasi kuanzia eneo la kiungo na kule mbele tunatakiwa kutengeneza nafasi zaidi lakini pia tutumie nafasi za kutosha,”alisema Nabi ambaye kwa mujibu wa msimamo wa ligi mpaka sasa ugenini amepata pointi saba kama Simba.

Nabi aliongeza kuwa mchezo wao dhidi ya Mbeya ambao hawajawahi kushinda nyumbani utakuwa ni fainali nyingine kabla ya kukutana na Simba.

Advertisement

“Nimewaambia wachezaji wetu hakuna mechi rahisi kwa Yanga na tunakutana na timu ngumu isiyojua kukata tamaa tunahitaji matokeo katika mchezo huu,”aliongeza Nabi ambaye ana sare moja ugenini na pointi tisa kwa mechi za nyumbani mpaka sasa


Advertisement