Msuva: Yanga kwanza

NYOTA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva ameguswa na namna ambavyo kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi anavyoonyesha dhamira ya kumhitaji kwenye kikosi chake.

Macho na masikio ya Nabi, Jumamosi ya wiki iliyopita yalikuwa yakimfuatilia mshambuliaji huyo alivyokuwa akifanya vizuri kwenye mchezo wa hisani kati ya timu ya Mbwana Samatta na Alikiba huku akicheza sambamba na nyota wake, Fiston Mayele.

Mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa yupo nchini kutokana na mgogoro wa kimaslahi na klabu yake ya Wydad Casablanca ambayo anamkataba nao hadi Juni 30, 2024 alisema Yanga ni nyumbani.

“Kama ningekuwa nataka kucheza mpira nyumbani ningekuwa tayari nimeshasaini kwa sababu nimefuatwa zaidi ya mara tano na viongozi wa klabu mbalimbali, ikiwemo Simba, Yanga pamoja na Azam, wameonyesha kunihitaji,”

“Napenda kuwa muwazi kuwa bado ninamalengo ya kuendelea kucheza mpira nje ya nchi ni vile tu hapa kati nimekumbana na changamoto ambazo zimenifanya kurejea nyumbani kwa muda lakini ninaimani kuwa haya ni mapito hivyo yatapita na maisha yataendelea,”

Nyota huyo alisema kama ataamua kurejea nyumbani basi anaweza kutoa kipaumbele kwa Yanga kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo lakini hilo haliwezi kumfanya kushindwa kuichezea Simba maana mpira ni kazi kwake.

“Yanga nina marafiki na ndio maana hata kipindi ambacho nimekuwa nikirudi nyumbani huwa naenda kuwatembelea pia ni klabu ambayo leo imenifanya kupiga hatua lakini pamoja na yote hii ni kazi yangu hivyo siwezi kutatizika na hilo,” alisema.

Katika mchezo wa hisani ambao Msuva alicheza sambamba na Mayele walikuwa upande wa timu Kiba na wawili hao walihusika kwenye bao la dakika ya 15 kiasi cha Nabi kuona anaweza kuwa na safu kali zaidi ya ushambuliaji kama atapata huduma ya nyota huyo.

Ilikuwaje? Beki wa Azam, Bruce Kangwa alipiga krosi, Mayele akaruka na mabeki wa timu Samatta, kisha mmoja wa mabeki hao kuugonga mpira Msuva akaunasa na kutupia nyavuni.

Zipo taarifa kuwa vigogo wa Yanga wapo tayari kutoa zaidi ya Tsh. 350 milioni ili kumrejesha kundini mshambuliaji huyo ambaye Nabi anaamini kuwa ataongeza makali kwenye safu yake ya ushambuliaji huku ikizingatiwa na ushiriki wao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua za awali.

Wydad Casablanca ambayo Msuva ameingia nayo kwenye mgogoro wa kimaslahi ndio mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga itaanzia hatua ya za awali, nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania anamchango kwenye ubingwa huo kwani kwenye michezo ya awali alicheza na kupachika mabao matatu na kutoa asisti mbili.

Yanga imepania kusuka upya kikosi chake ikiangalia zaidi michuano ya kimataifa inayokwenda kuanza wikiendi ya kwanza ya Septemba mwaka huu kwenye viwanja mbalimbali.