Msuva ni laki 5 kwa siku

Msuva ni laki 5 kwa siku

MAISHA anayoishi mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva kwa sasa huko Morocco ni ya kifahari tangu ajiunge na miamba ya soka nchini humo Wydad Casablanca ni kama ameingia anga za maisha ya nyota wakubwa wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya.

Tangu Msuva aliporejea Morocco ambako anacheza soka la kulipwa kwa ajili ya kuanza maisha yake mapya kwenye klabu hiyo ambayo ilimsajili akitokea Difaa El Jadida kwa Tanzania ni kama mchezaji ambaye ametoka mkoani kwenda Simba au Yanga.

Wydad Casablanca ambao ni miongoni mwa klabu tajiri kwa Afrika, imeona Msuva afikie na kukaa kwenye Hoteli ya kifahari nchini humo iitwayo Grand Mogador City Center Casablanca na inaelezwa analipiwa zaidi ya laki tano (Tsh 577,823) kwa fedha za Kitanzania kwa siku moja.

Leo Msuva amefikisha siku ya tisa kwenye Hoteli hiyo tangu atue Morocco akitokea Tanzania katika majukumu ya timu ya taifa na mapumziko ya msimu maana nchini humo ndio ulikuwa umemalizika. Sasa piga hesabu mpaka sasa ni zaidi ya milioni tano ametumia.

Hayo ndiyo maisha ambayo hata wachezaji wa Machester United wamekuwa wakiishi, kabla ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG, mastaa wa timu hiyo waliweka kambi kwenye Hoteli ya Hilton Manchester Deansgate ambayo kichwa kimoja kulala inaendana na kiasi ambacho Wydad Casablanca inamlipia kwa siku Msuva.

MSIKIE MSUVA

“Maisha ni tofauti kabisa kwa sasa nipo mjini aisee na hata wakati nikiwa Difaa sikuwa mtembeaji zaidi ya kukaa ndani na nikitembea basi nipo na timu, huwa kuna gari limekuwa likinichukua muda wa kwenda mazoezini na kunirudisha kila siku,” alisema na kuendelea.

“Nimepokewa vizuri na hata mazoezi yao inaonyesha kuwa hii ni klabu kubwa naamini nitacheza kwa mafanikio. Sijajua kama maisha yangu yatakuwa hapa au watanitafutiwa nyumban kama ilivyokuwa Difaa,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga.

BY ELIYA SOLOMON