Mpole amshusha Minziro presha

Mpole amshusha Minziro presha

Dar es Salaam. Bao moja lililofungwana kinara wa mabao msimu uliopita, George Mpole limemuibua kocha wake, Fredy Minziro, ambaye amesema litapunguza presha eneo lake la ushambuliaji.

Minziro alisema hayo wakati kikosi chake kikijiandaa kwa mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania, utakaofanyika Oktoba 4.

Mpole, ambaye alifunga mabao 17 msimu uliopita, alifungua akaunti ya mabao dhidi ya Singida Big Stars na kuisaidia timu yake kuambulia pointi moja kwenye mchezo huo kwa sare ya 1-1.

Akizungumza jana, Minziro alisema safu yake ya ushambuliaji ilikosa utulivu, lakini baada ya nyota wake kupata nafasi ya kufunga ameshusha presha ya maneno mengi dhidi yake.

“Mpole kufunga kwangu na kwa timu kwa ujumla kumepunguza presha, naamini mchezo ujao utakuwa na ushindi mkubwa kwetu washambuliaji wangu hawata niangusha hilo nimeanza kuliona kuanzia mazoezini wananionyesha wana uchu wa kufunga.

“Tutakuwa ugenini lakini sina wasiwasi na vijana wangu, baada ya kuondolewa kimataifa waliumia sana na kuniahidi kufanya vizuri kwenye ligi na Kombe la Shirikisho la Azam ili kusaka nafasi nyingine msimu ujao,” alisema.

Minziro alisema kikosi chake kinaendelea vizuri na mazoezi kuelekea mchezo huo, muda na siku yoyote watafunga safari kuifuata Polisi Tanzania.