Morrison bado ni yuleyule

Dar es Salaam. Licha ya kufungua vizuri Ligi msimu huu, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison hajawa na uhakika wa kucheza mechi mfululizo kwenye kikosi cha timu hiyo.

Morrison amejiunga na Yanga msimu huu akitokea Simba na matarajio ya viongozi na mashabiki wengi wa timu hiyo yalikua yakimuona akifanya vizuri na kuisaidia timu kwenye Ligi na kimataifa lakini mwisho wa siku kwenye Ligi hajawa sehemu ya kikosi chao mara kwa mara.

Kiungo huyo kwenye mechi 13 ambazo Yanga imecheza, yeye amecheza mechi nne tu na kufunga mabao mawili huku moja likiwa ni la penalti.

Morrison katika mechi hizo nne amecheza dakika 273 tu licha ya usajili wake kuwa sehemu kubwa na gumzo kutokana na kutokea upande wa wapinzani wao (Simba).

Kiungo huyu alianza kucheza ligi mchezo dhidi ya Polisi Tanzania akiingia dakika ya 57 kuchukua nafasi ya Dickson Ambundo, alianza dhidi ya Coastal Union na alifunga bao kwenye mchezo huo kabla ya kutolewa dakika ya 72, akimpisha Farid Mussa.

Alianza pia dhidi ya Geita Gold na alifunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti na kutolewa dakika ya 80, nafasi yake kuingia Jesus Moloko.

Mchezo wake wa mwisho kuonekana uwanjani ni dhidi ya Singida Big Stars, akitumia dakika 64 kabla ya kumpisha Tuisila Kisinda, kisha kudaiwa kuwa na matatizo ya kifamilia.

Wadau wa soka wamedai Morrison ni kama anaitia hasara Yanga kutokana na kushindwa kuwa sehemu ya kikosi mara kwa mara.

Mshambuliaji wa zamani Tanzania Prisons na Yanga, Herry Morris alisema Morrison anatakiwa kutuliza akili na kucheza mpira kwani uongozi umemuamini.

“Anatakiwa atulie na kucheza, akiituliza akili na kutunza nguvu zake atafanya vizuri kwa sababu wote tunajua uwezo wake.

“Viongozi ni kama wazazi wanatakiwa wawe naye karibu, wamtengeneze kisaikolojia, wazungumze ili acheze mpira,” alisema Morris.

Mchezaji wa zamani wa Yanga na Simba, Zamoyoni Mogela alisema Morrison hajabadilika na ameendelea kuwa ni yule yule wa siku zote akimtaja kama mtovu wa nidhamu.

“Hajabadilika na kubwa zaidi ni nidhamu, ni mchezaji wa kigeni anatakiwa kubadilika,” alisema Mogela.

Morrison yupo katika mwaka wa kwanza kati ya mwili aliyosaini kucheza Yanga.