Mkwanja Yanga, Tusker kicheko

Mkwanja Yanga, Tusker kicheko

SASA ni rasmi Kenya na Tanzania Bara wameshapata mabingwa wa ligi zao kwa msimu 2021/22 lakini kuna tofauti kubwa kwenye zawadi ya kifedha ambazo mabingwa wanapokea.
Tusker FC walikua katika ubora wao hususan mzunguko wa pili Ligi Kuu Kenya na kufanikiwa kuwapiku Kakamega Homeboyz kwa unafuu wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa baada ya timu zote kufungamana kwa pointi 63.
Napo katika nchi jirani ya Tanzania, katikati mwa wiki hii, Yanga waliifunga Coastal Union mabao 3-0 na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara waliyokosa kwa miaka minne huku wakiwa bado na mechi nne kumaliza msimu.
Licha ya Yanga na Tusker FC wote kusherehekea ubingwa, kuna pengo kubwa ya fedha ambazo wanaingiza kibindoni.
Fedha ambayo watapokea Tusker FC inayonolewa na mzawa mkongwe Robert ‘Simba’ Matano kama wangekuwa wanashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara basi ni zawadi ya fedha anazopewa timu itakayomaliza nafasi ya 10.
Kamati ya Mpito ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) iliyoteuliwa na Serikali imetenga kiasi cha Shilingi milioni mbili atakazokabidhiwa bingwa wa Ligi Kuu Bara na katika mantiki hii ni Tusker FC waliofanikiwa kutetea taji lao.
Msimu uliopita, Tusker FC waliowapiku KCB mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Kenya walipokea Shilingi milioni tano ambayo ilitolewa na uongozi wa FKF uliobanduliwa ofisini wake Nick Mwendwa.
Wakati Tusker FC akiondoka na Shilingi milioni mbili, Yanga wanasubiri kukabidhiwa Shilingi milioni 30 (sawa na Shilingi milioni 600 za Tanzania).
Kiasi hiki kikubwa cha fedha atakachopata Yanga kinatokana na utiriri wa wadhamini ambapo mbali ya Ligi Kuu Tanzania Bara kujivunia kuwa na mdhamini mkuu ambayo ni kampuni ya benki, takribani mechi zote za ligi hiyo zinaonyeshwa mubashara na timu zote zilizoshiriki zitaondoka na fedha tofauti na Kenya ambapo ni mshindi tu ndiye mwenye uhakika pochi lake kuwa nene.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ilitangaza jumla ya Shilingi milioni 90 zitatolewa kama zawadi kwa timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo ambayo inatarajiwa kufika tamati mwishoni mwa mwezi huu.
Wakati bingwa Tanzania akiondoka na Shilingi milioni 30, mshindi wa pili atakabidhiwa Shilingi milioni 15 na timu itakayoshika nafasi ya tatu kuweka kibondoni Shilingi milioni 12 huku timu zingine zitakazomaliza kuanzia nafasi ya nne hadi 16 hazitaondoka kapa kwasababu kila timu imetengewa fedha.
Timu mbili ambazo zinashuka daraja kila moja zimetengewa Shilingi milioni 10 na pia kuna Shilingi milioni 20 kwa timu yenye nidhamu.