Mastaa: Gomes fundi sana

KOCHA mkuu wa Simba, Didier Gomes amefanya vitu vilivyotikisa mioyo ya wachezaji wa zamani ambao wamemganda wakimwona kama tegemeo na mtu sahihi wa kuifikisha mbali klabu hiyo.

Kati ya vitu vilivyowavutia kwa Gomes, ni nidhamu, uwezo wa timu, upangaji mzuri wa kikosi na kutokufanya kazi kwa mazoea ikiwamo ya kuangalia ni staa gani anapendwa na mashabiki ndiye apangwe hata kama hana uwezo.

Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima alisema Gomes ameibadilisha timu katika maeneo makuu mawili, timu kumiliki mipira na kuwapanga wachezaji kutokana na uwezo wao na sio kwa kelele za mashabiki waliokariri wachezaji wenye majina makubwa ndio wanaostahili kucheza hata kama viwango vyao vipo chini.

“Simba hii inacheza kitimu. Inashambulia na inakaba kwa pamoja, tofauti na kocha aliyepita Sven, mchezaji alikuwa akinyang’anywa mpira basi unakaa muda mrefu kwa mpinzani. Niliona hilo kwa Clatous Chama ila sasa amebadilika anacheza na kukaba;

“Ameleta nidhamu kwa wachezaji kuheshimu kazi kwa kuzingatia miiko ya soka, lingine kuna kipindi Cris Mugalu alikuwa anapigiwa kelele na mashabiki kutokupangwa ila kwa sasa kocha kaona anafaa kwenye mfumo wake anampanga, wanapiga kelele kwa Meddie Kagere tena, hii inaonyesha ni kocha mwenye maamuzi,” alisema.

Alisema ubora wa Simba kwenye ligi hadi Caf unatokana na Gomes kufanikiwa kuwatumia wachezaji kuendana na mifumo yake wanayofiti, anakuwa na uhakika wa kupata matokeo muda wowote anaotaka.

“Nimeona anavyofanya mabadiliko unaona kabisa ni kocha anayejua anataka nini na ameusoma mchezo, akiingia mchezaji fulani anakwenda kufanya kitu, ama akikosekana mchezaji wake wa kikosi cha kwanza anajua kuziba pengo la nani aanze na nani,” alisema.

Hoja yake iliungwa mkono na beki wa zamani wa Simba, Kasongo Athuman na alisema; “Nimecheza kwa mafanikio makubwa kwa hiyo naelewa kwa nini baadhi ya wachezaji wanasugua benchi mbele ya Gomes hasa baada ya kuhudhuria mazoezi yao, ni kocha anayeamini katika kanuni za soka.”

“Hayumbishwi na kumpanga mchezaji kwa mazoea ya kupendwa na mashabiki, hiyo ndio tofauti niliyoiona baina yake na Sven na akiendelea hivyo Simba itakuwa mfano wa kuigwana timu nyingine kuwa na kikosi kinachoshindana,” alisema.

Beki wa zamani wa timu hiyo, William Martin alisema; “Kila kocha alikuwa na ufundi wake kwa maana ya Sven alifanya alipoishia, pia Gomes unaona kabisa jinsi timu ilivyokuwa inacheza kwa kujiamini michuano ya Caf naamini akikaa na timu muda mrefu ataifikisha mbali.”