Mashabiki safi, Polisi yaitangulia Simba Kirumba

Muktasari:

Polisi walifika mapema na kukutana zomeazomea ya mashabiki wa Simba, huku Wekundu wakitua dakika 20 baadaye.

Mwanza. Katika kuhakikisha wadau na mashabiki wa soka wanapata burudani bila bughudha, jumla ya milango mitatu imefunguliwa ili kuondoa usumbufu.

Hadi sasa tayari mashabiki wanaendelea kumiminika katika uwanja wa CCM Kirumba ambapo milango ilifunguliwa mapema tangu saa 5 asubuhi ili kuruhusu uingiaji kwa mashabiki na wadau kuziona Simba na Polisi Tanzania.

Hii ni tofauti na siku nyingine ambapo huwa inafunguliwa mlango mmoja na kusababisha hekaheka kwa mashabiki hata wasimamizi.

Wakati huohuo, Polisi Tanzania imekuwa ya kwanza kuingia uwanjani baada ya kuwasili saa 8:07 mchana huku wakikutana na zomeazomea ya mashabiki wa Simba.

Timu hiyo ambayo ilikuwa imezingirwa na Askari Polisi, walishuka kwa kujiamini na kwenda hadi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji.

Simba wao walutua saa 8:28 mchana na kupokelewa na shangwe za mashabiki wao ambao wamefurika kwenye jukwaa la vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji.