Mashabiki Bandari wataka wachezaji wajitolee zaidi

Mashabiki Bandari wataka wachezaji wajitolee zaidi

MOMBASA. WAPENZI wa Bandari FC wamewaomba wachezaji wao wahakikishe wanapata ushindi kwenye mechi yao ya Ligi Kuu ya FKF dhidi ya Kariobangi Sharks ambayo itachezwa jijini Nairobi siku ya Jumapili.

Kwa niaba ya mashabiki na washika dau wa soka wa Mombasa na Pwani, Mkurugenzi wa Cosmos FC Aref Baghazally amesema wana imani kubwa timu yao kufanya vizuri dhidi ya Kariobangi na akawataka wachezaji wacheze kwa kujitolea kuihami timu yao.

“Mechi nyingi zinazohusisha sisi na Sharks huwa zinamalizikia kwa sare lakini kutokana na jinsi timu yetu ilivyo katika fomu nzuri, tuna imani kubwa wanasoka wetu watatupa furaha kwa kupata ushindi,” akasema Baghazally.

Aliyekuwa mchezaji wa klabu ya Horohoro FC ya Lamu, Ali Basalama amesema wanawategemea wanasoka wa Bandari kushinda mchezo huo na mechi nyingine zilizobakia kwani kuna uwezekano wa kuwa mabingwa wa msimu huu.

“Tuna matumaini makubwa kwa jinsi timu yetu inavyocheza soka la hali ya juu, tutaweza kuwashinda Kariobangi na vijana wetu kurudi Mombasa wakiwa wametia kibindoni alama zote tatu,” akasema Basalama.

Na aliyekuwa mwanasoka wa timu ya Mwenge FC Said Badi amesema wangelifurahikia kusikia timu hiyo ya Bandari inaobuka washindi wa Ligi Kuu ili iweze kushiriki kwenye Ligi ya Klabu Bingwa barani Afrika.

Lakini kutokana na hali ilivyo wakati huu, Bandari ama timu yoyote ikishinda, haitakubaliwa kushiriki soka hilo la barani kutokana na marufuku nchi yetu iliyopigwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

“Ningeliomba Waziri wa Michezo Amina Mohamed afuatilize mwenyewe juu ya marufuku tuliyopigwa na hata asafiri hadi makao makuu ya Fifa kutaradhia kurudishwa mashindanoni. Lakini tukingoja kuambiwa, tutabakia na marufuku hii kwa kipindi kirefu,” akasema Badi.