Makocha Yanga wabeba lawama

Wednesday January 12 2022
Makocha PIC
By Mwanahiba Richard

Zanzibar. Benchi la ufundi la Yanga limekiri kuwa linawajibika kwa mabadiliko ya kipa lililofanya katika mchezo dhidi ya Azam FC juzi ambao walipoteza kwa mikwaju ya penalti 9-8 katika Uwanja wa Amaan kwenye nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Zikiwa zimebaki dakika chache kabla ya mchezo kumalizika, Yanga ilimtoa kipa Abuutwalib Mshery na kumuingiza Erick Johora kuchukua nafasi yake, ikionekana ililenga kufanya vizuri katika hatua ya kupigiana mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa suluhu.

Hata hivyo, Johora aliyeonekana hakuwa fiti alifungwa penati zote tisa na wachezaji wa Azam na kuifanya Yanga itupwe nje ya mashindano hayo sambamba na kutema ubingwa iliokuwa ikiutetea.

Kocha Kaze alisema yeye ndiye anapaswa kulaumiwa kwa mabadiliko hayo aliyoyafanya ingawa anaamini yalikuwa kwa nia njema.

“Johora sio kipa mbaya nilifanya mabadiliko hayo kwa kujalidiliana na wenzangu pamoja na wachezaji wenyewe wakati wa mazoezi kuwa kama tutafika kwenye penalti basi atadaka Johora na alifanya vizuri zaidi mazoezini.

“Niseme tu kuwa napokea lawama hizo kwani mimi ndiye kocha ambaye nilifanya mabadiliko hayo yaliyoigharimu timu, ila kwenye upigaji wa penalti lolote linaweza kutokea kikubwa tulitakiwa kumaliza mchezo ndani ya dakika 90 lakini tulikutana na ushindani mkubwa kwani hata wapinzani wetu walijiandaa vizuri.

Advertisement

“Dakika 20 za mwisho kipindi cha kwanza tulifanya vizuri zaidi lakini kipindi cha pili wachezaji walikosa utulivu hivyo tunawapongeza Azam na tunaenda kujipanga kwenye ligi ili tuendelee kuwa juu ya msimamo malengo yetu ya huku yamepotea ila bado kwenye ligi na mengine tunayo. Hatujawakwepa Simba ila wakati mwingine matokeo yanakuwa hivi na lazima mshindi apatikane,” alisema Kaze.

Kocha wa makipa wa Yanga, Razack Siwa alisema kuwa anaamini hofu ndio ilimwangusha Johora na si vinginevyo.

“Johora alijua kabisa kuwa ikifika penalti yeye analazimika kukaa golini kwani ndiye alifanya vizuri zaidi mazoezini, kutokuwa na utimamu wa mwili kwasababu hachezi mechi sio sababu kubwa sana ila wakati mwingine kwenye hizi timu kunakuwa na presha pengine alipatwa na hilo ndio maana hakuonyesha ubora.

“Kama makocha hatuwezi kukwepa lawama na Yanga ya sasa inahitaji matokeo mazuri na sio wachezaji wa kujaribu mechi zenye ushindani na kuhitaji ushindi,” alisema Siwa.

Advertisement