Mabadiliko Yanga kumekucha

Mabadiliko Yanga kumekucha

Muktasari:

Yanga imeazimia kufanya mabadiliko katika uendeshaji wa klabu hiyo.

Dar es Salaam. Rasimu ya awali ya mchakato wa mabadiliko ya Klabu ya Yanga umewasili kutoka Hispania na tayari kwa kwa ajili ya kupitia mapendekezo yaliyokuwamo.

Hafla fupi ya makabidhiano hayo imefanyika jana jijini Dar es Salaam katika hoteli ya Serena na Mwenyekiti wa Kamati ya Mabadiliko, Wakili Alex Mgongolwa ameikabidhi kwa uongozi kupitia mwenyekiti, Mshindo Msolla.

Akizungumza katika makabidhiano hayo yaliyowahusisha wanachama wakongwe na viongozi wa zamani jana, Mgongolwa alisema baada ya vikao mbalimbali na kampuni ya La Liga, ambayo ndiyo iliyopewa kazi ya kusimamia mchakato huo, ripoti kamili iliwasilishwa kwao.

Mgongolwa alisema ripoti hiyo ya kurasa 400 iliyofuatwa na mjumbe wa kamati yao, Mhandisi Hersi Said, imekuja na ushauri wa mfumo wa uongozi ambao utatumika katika klabu yao.

Hata hivyo, Mgongolwa alisema katika ushuri huo yapo mambo mawili waliyozingatiwa katika kutafuta ushauri, ambao kubwa ni kuifanya nguvu kubwa ya klabu kubaki kwa wanachama kama ambavyo wamekuwa wakiita ‘timu ya wananchi’.

“Hatua ambazo tulizianza baada ya kupewa hii kazi sisi kama kamati ilikuwa ni kutazama ukubwa wa hii kazi nakumbuka niliwahi kueleza hili huko nyuma,” alisema Mgongolwa.

“Baada ya mchakato mrefu tulimpata mganga, ambaye atakuja kutibu matatizo yetu, ambaye alikuwa ni hawa Laliga na tukasaini naye makubaliano katika kuifanya hii kazi.

“Tulipowapa hii kazi vipaumbele vyetu viwili vilikuwawatusaidie katika chakato mzima wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji na kiungozi na kitu kingine tuliona Yanga imejikita katika dhana ya umiliki wa wananchi na ndiyo maana huwa tunaita timu ya wananchi.

“Hapa lengo lilikuwa tunataka kuwafanya wanachama na mashabiki kutafuta namna ambayo wataweza kujihusisha na klabu yao moja kwa moja na ili wawe sehemu ya klabu tofauti na zile klabu zinazojiendesha kibiashara.

“Yanga ina matawi ambayo yanawanachama na mashabiki lengo letu hapa hatukutaka tutafute mfumo ambao tutawaacha hawa watu wetu nje ya mfumo ambao tunataka kwenda nao.

“Wenzetu hawa Laliga waliposikia hayo kama ndio vipaumbele wakasema watatupa jopo la wataalam ambao watasimamia kazi hii.

Mara baada ya makabidhiano hayo Msola alisema mara baada ya uongozi wao kupokea ripoti hiyo wao wataipeleka kwa mshauri wao wa kiungozi Senzo Mbata ambaye atakwenda kuichambua kazi ambayo watashirikiana na kamati ya utendaji.

Msola alieleza kwamba baada ya kamati yao ya utendaji na Senzo kuichambua pia itaundwa kamati ndogo ya mabadiliko ya katiba ambayo itakwenda kusimamia mabadiliko ya katiba yao kulingana na ushauri wa kwenye ripoti husika.

By Khatimu Naheka