Kombe lampa mwanya Kaze

Dar es Salaam. Ubingwa wa Kombe la Mapinduzi ambao Yanga imechukua umetajwa kuwa utaongeza morali katika kikosi hicho msimu huu, huku wadau wakitaka kocha Cedrick Kaze aachwe afanye majukumu yake.

Yanga ilitwaa ubingwa wa Mapinduzi Januari 13 kwa kuwafunga watani zao wa Jadi, Simba kwa penalti 4-3 kufuatia suluhu ndani ya dakika 90.

Hiyo inakuwa mara ya pili kwa Yanga kutwaa ubingwa huo wa michuano hiyo baada ya miaka 14 kupita tangu walipofanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 2007 kwa kuifunga Mtibwa Sugar kwenye fainali.

Yanga pia inakuwa ni mara ya kwanza kuifunga Simba katika mashindano hayo kwani mara mbili ilijikuta ikilala mbele ya watani zaoi. Janurai 12, 2011 kwenye mchezo wa fainali ilifungwa mabao 2-0 wakati Januari 10, 2017 ilipoteza mchezo mbele ya Wekundi wa Msimbazi kwa kuchapwa kwa penalti 4-2 baada ya suluhu ndani ya dakika 90.

Yanga iliwasili kwa mbwembwe jana mchana ikitokea Zanzibar, huku ikipolkelewa na mashabiki lukuki.

Msafara wa mabingwa hao ulitoka bandarini na kupita katika mtaa wa Msimbazi, makao makuu ya watani zao, Simba, kisha kuwenda hadi Jangwani.

Kocha Kaze aliwaahidi mashabiki waliokusanyika kuwapokea kuwa wakati umefika wa wao kutembea vifua mbele.

“Wakati wa unyonge umekwisha, mnatakiwa kujivunia timu yenu na mjitokeze kwa wingi katika kila mchezo wetu kwasababu timu ipo imara,” alisema Kaze.

Kwa misimu mitatu, Yanga imejikuta ikiitazama tu Simba ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na msimu huu imeonekana kuwa inataka kurudisha heshima yake kwani hadi sasa ndiyo timu ambayo haijapoteza mchezo kwenye ligi hiyo, huku ikiongoza ligi ikiwa na pointi 44 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 35.

Mchambuzi Ally Mayay alisema kitendo cha Yanga kutwaa ubingwa wa Mapinduzi kitakuwa msasa mkubwa kujenga saikolojia ya wachezaji wa timu hiyo hivyo kuwachocheza zaidi kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu.

“Timu inapofanikiwa kutwaa kombe inakuwa msaada mkubwa kisaikolojia kwa wachezaji.Ubingwa huo tena kwa kumfunga mtani wa jadi utawaongezea wachezaji wa Yanga kujiamini zaidi katika mapambano yao ya ubingwa kwenye ligi ambao wameukosa kwa miaka mitatu.

“Hali hiyo itawapa morali ya kujua kuwa kumbe wakiongeza juhudi wanaweza kurejesha heshima yao ya kutokuwa mabingwa wa ligi kwa muda mrefu,” alisema Mayay.

Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima’ Jembe Ulaya’ alisema kuchukua ubingwa mbele ya Simba ni jambo zuri ambalo litawachochea wachezaji wa timu hiyo kufanya vizuri zaidi kwenye ligi.